January Makamba Ataja Mambo 4 Yaliyompa Ushindi Ndugulile Ukurugenzi WHO

 

January Makamba Ataja Mambo 4 Yaliyompa Ushindi Ndugulile Ukurugenzi WHO

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amempongeza Dk Faustine Ndugulile kwa kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Ukanda wa Afrika.


Dk Ndugulile ambaye ni Mbunge wa Kigamboni (CCM), jijini Dar es Salaam amechaguliwa jana Jumanne, Agosti 27, 2024 katika Mkutano wa Afya wa 74 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaoendelea Brazzaville, Congo.


Wagombea wengine walikuwa ni Dk Boureima Hama Sambo (Niger) Dk N'da Konan Michel Yao (Cote d'Ivoire) Dk Ibrahima Soc'e Fall (Senegal) na Dk Richard Mihigo (Rwanda).


Dk Ndugulile amepata ushindi huo baada ya nchi 19 kuipigia kura Tanzania katika mzunguko wa kwanza, 12 Senegal, huku Niger na Rwanda zikipigiwa kura saba kila moja.


Baada ya kutangazwa mshindi, pongezi zimeendelea kumiminika na Watanzania mbalimbali akiwemo January ambaye kabla ya uteuzi wake kutenguliwa Julai 21, 2024 na nafasi yake kuteuliwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alishiriki kwenye kampeni.


Katika kurasa zake za kijamii, January ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM) ameelezea mambo manne yaliyochagiza ushindi huo wa Dk Ndugulile anayekwenda kuongoza nafasi hiyo na kuwa mtu wa kwanza wa ukanda wa Afrika Mashariki kushika wadhifa huo.


January ameandika:"Hongera Dk. Faustine Ndugulile kwa ushindi ulioiletea heshima nchi yetu. Mambo manne yametubeba:- sifa na uwezo wako binafsi, sapoti kubwa ya Mhe Rais na Serikali, heshima ya Tanzania Barani Afrika na kampeni mahiri. Pongezi kwa wote walioshiriki kampeni. Tunakutakia kila la heri."

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad