Miguel Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga ameweka wazi kuwa wachezaji wapya ndani ya kikosi hicho wanaelewa haraka jambo ambalo linawafanya wawe tayari kwa msimu wa 2024/25.
Yanga iliweka kambi kwa muda nchini Afrika Kusini ambapo huko ilialikwa kwa ajili ya mechi za kirafiki ilitwaa Kombe la Toyota Cup kwa ushindi mbele ya Kaizer Chiefs kwa ushindi wa mabao 4-0.
Mabao hayo yalifungwa na Prince Dube ambaye ni mshambuliaji mpya aliibuka hapo baada ya kumalizana na mabosi wake wa zamani Azam FC, mabao mawili yalifungwa na Aziz Ki mwenye tuzo ya MVP msimu wa 2023/24 na moja mali ya Clement Mzize.
Katika kilele cha Wiki ya Mwananchi, Agosti 4 2024 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Yanga 2-1 Red Arrows kwa mabao ya Mudathir Yahya na Aziz Ki na bao la Red Arrows lilifungwa na Ricky Banda.
Gamondi amesema; “Wachezaji wapya waliopo ndani ya kikosi wanaelewa haraka na hilo linafanya waingie kwenye mfumo mapema na tumekuwa na mwendelezo mzuri kwenye mechi ambazo tunacheza.
“Unaona kwenye mchezo wetu dhidi ya Red Arrows namna ilivyokuwa kila mmoja ameonyesha kitu kizuri na tulipata upinzani mkubwa kutoka kwa wapinzani wetu.”
Mbali na Dube pia kuna Clatous Chama mchezaji wa kwanza kutambulishwa Yanga baada ya kusajiliwa ilikuwa ni Julai Mosi 2024, Duke Abuya, Boka Chadrack.