HUYO Gamondi atafanya watu wasiingize timu uwanjani. Unaweza kusema hivyo baada ya kocha wa Yanga, Miguel kuweka wazi kuwa anaendelea kuwafungia kazi safu yake ya ushambuliaji kuwa makini.
Safu ya ushambuliaji ya Yanga inaongozwa na Kennedy Musonda, Clement Mzize na Prince Dube ambaye amekuwa na kiwango bora cha kufumania nyavu toka asajiliwe msimu huu.
Gamond amesema katika michezo miwili ya ushindani waliocheza hivi karibuni fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC na Ligi ya Mabingwa Afrika na Vital ‘O walipata mabao mengi lakini walipoteza nafasi ambao wangekuwa makini wangeshinda zaidi ya bao 5.
Yanga Jumamosi Agosti 17, 2024, ilicheza mechi ya mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika na Vital’ O kwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi Dar-es-Salaam.
Gamondi amesema anafurahi kuona wanaendeleza walipoishia kwa kufanikiwa kufunga idadi ya mabao mengi lakini anaamini wanapoteza nafasi nyingi anarudi kwenye uwanja wa mazoezi kufanyia kazi.
“Tumekuwa bora katika maeneo mengi, tumecheza vizuri na kutengeneza nafasi na kufunga, bado tunaitaji kuimarisha zaidi eneo la ushambuliaji kuhakikisha tunaweza kutumia vizuri nafasi na kuwa mabao,” amesema kocha huyo.
Kuhusu mshambuliaji wake, Clement Mzize amesema amekuwa na kiwango bora na kusaidia timu hiyo kufikia malengo yao katika mashindano ya ndani na kimataifa.
“Kila siku amekuwa na kiwango bora, kushirikiana na washambuliaji waliopo ndani ya timu tutafikia malengo ikiwemo kufikia pale tulipoishia msimu uliopita na kucheza fainali ya Afrika,” amesema kocha huyo.