WAKATI Rais Samia Suluhu Hassan, akiwataka wanachama na mashabiki wa Simba kusahau yaliyopita na sasa kuganga yajayo, Kocha Mkuu Fadlu Davils, amesema baada ya mechi ya juzi dhidi ya APR sasa wapo tayari kwa Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga, Alhamisi ijayo kwenye Ngao ya Jamii.
Akizungumza juzi wakati wa Tamasha la Simba Day kupitia simu ya mkononi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, Rais Samia aliusalimia umati wa mashabiki zaidi ya 60,000 uliofurika Uwanja wa Benjamin Mkapa, akiwataka kusahau yote yaliyopita na kuangalia nini watafanya kwa msimu huu.
Msimu uliopita, timu ya Simba haikufanya vema kwenye michuano mbalimbali, ikiishia njiani kwenye Kombe la FA, pamoja na kumaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, ambayo imewanyima tiketi ya kwenda Ligi ya Mabingwa na badala yake msimu ujao itacheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika salamu zake hizo, rais ambaye mwaka jana alikuwa mgeni rasmi kwenye Simba Day huku mwaka huu akisema ameshindwa kuhudhuria kutokana na shughuli na ziara za kikazi, ingawa hata hivyo haikumzuia kuangalia tamasha hilo kwenye televisheni.
"Nawashukuru sana, nimerudi ziara sasa hivi nimefungua TV nimeona uwanja umejaa na shughuli zinaendelea. Nakumbuka mwaka jana tulikuwa sote hapo, lakini mwaka huu, limenipita lakini nikaona lisinipite kabisa kabisa mpaka niongee nanyi," alisema Rais Samia, ambaye alikuwa anasikika kupitia simu ya Msigwa na kushangiliwa na maelfu ya watazamaji waliokuwa uwanjani hapo.
Katika mechi hiyo, Simba iliichapa APR ya Rwanda mabao 2-0, yaliyowekwa wavuni na Debora Fernandes Mavambo kwa shuti kali la mbali, na Edwin Balua kwa mkwaju wa faulo, baada ya Valentino Mashaka kuangushwa nje kidogo ya eneo la hatari.
Mara baada ya mchezo huo, Kocha wa Simba, Fadlu, alisema sasa akili yake anaielekeza kwenye mchezo wa Alhamisi dhidi ya Yanga, akisema amewatazama wapinzani wake katika michezo kadhaa waliyocheza nchini Afrika Kusini.
"Tulikuwa na wiki nne za maandalizi, ingawa bado wachezaji wangu miguu ni mizito kutokana na mazoezi magumu waliyokuwa wakiyafanya, lakini bado haiondoi ukweli kuwa tunakabiliana na mechi ngumu na tuko tayari kwa dabi, nimeiona Yanga ikicheza mechi zake Afrika Kusini, hivyo tunakwenda kujiandaa," alisema.
Akizungumzia mchezo wa juzi, alisema kipindi cha kwanza hakikuwa kizuri sana kutokana na jinsi wachezaji wake walivyokuwa wakicheza, lakini alifurahishwa na kile alichokiona kipindi cha pili.
"Kipindi cha kwanza tulicheza pasi za taratibu, halafu ni nyingi bila kufanya mashambulizi haraka langoni mwa mpinzani, kipindi cha pili baada ya kuwaelekeza wachezaji wangu kwamba nini tunatakiwa tufanye, kuondoka na mpira haraka, kushambulia, kuwaweka wapinzani kwenye presha na ndicho tulichofanya," alisema raia huyo wa Afrika Kusini.
Kocha Mkuu wa APR, Mserbia Darko Novic, alikisifu kikosi cha Simba, akisema Afrika itashuhudia kikosi bora msimu huu.
"Kiukweli kabisa Simba ni timu nzuri, iko bora sana, nimeona ni wazuri kwenye fiziki, wanaelewana, wanaweka mpira chini na pasi nyingi muda wote na nafikiri msimu huu itaionyesha Afrika kuwa ni timu ya kipekee," alisema.
Alisema timu yao imepoteza mechi hiyo kutokana na aina ya mpinzani waliyekutana naye na si vinginevyo.
"Nimepata upinzani mkubwa hasa kipindi cha pili, na kuna vitu vingi vilivyosababisha tupoteze mechi, nimeona leo vijana wangu hawakuwa na maelewano, muunganiko, kuwakuwapa presha wapinzani wetu kwa mashambulizi makali kama kawaida yetu, lakini najua ni kwa sababu tumecheza na timu nzuri kuliko sisi, ina wachezaji bora wenye uzoefu katika michezo mbalimbali ya kimataifa," alisema kocha huyo ambaye timu yake inatarajia kukutana na Azam FC, katika mechi ya hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika.