Zikiwa zimebaki saa nane kabla ya wana Simba kushuhudia kikosi kipya cha msimu wa 2024/25, hapa Benjamin Mkapa Ubaya Ubwela ni mwingi, hii ni baada ya jezi nyekundu na nyeupe kutapakaa karibu kila kona nje ya uwanja.
Rangi hizo ndizo zinazotumiwa zaidi na Simba katika jezi za klabu hiyo, jambo linaloashiria mashabiki wa timu hiyo wapo tayari kushuhudia kikosi chao cha msimu mpya kwani mapema zaidi wameanza kuingia uwanjani.
Foleni ni ndefu mageti yote ya kuingilia uwanjani mashabiki kibao waliojitokeza wanahimizana kuingia ndani kwa utaratibu tayari kwa ajili ya kuishuhudia timu yao.
Hakika huu ni Ubaya Ubwela kama wao wanavyosema, Wanasimba wapo na furaha huku vikundi mbalimbali vya ushangiliaji vikionekana kuanza kazi mapema.
Mwanaspoti limeshuhudia mashabiki wa Simba wakipanga mistari zaidi ya minne katika kila geti wakitaka kuwahi kuingia ndani kushuhudia burudani mbalimbali sambamba na chama lao likijipima nguvu dhidi ya APR kutoka Rwanda ukiwa ni msimu wa 16 tangu tamasha hilo limeanzishwa mwaka 2009.
YANGA WAMO
Achana na nyomi ya mashabiki wa Simba waliofurika kwa Mkapa, unaambiwa Yanga pia wameibuka kushuhudia shoo ya watani wao.
Mashabiki wachache waliovaa jezi za Yanga wameonekana wakiingia uwanjani hapo kushuhudia Mnyama akitambulisha kikosi chake ambacho kwa asilimia kubwa ni wachezaji wapya kutokana na kufanya usajili wa nyota 14 wanaokwenda kuitumikia timu kwa mara ya kwanza.