Kylian Mbappe Aweka Rekodi Mpya Real Madrid....

 

Kylian Mbappe Aweka Rekodi Mpya Real Madrid....

Kylian Mbappe jana alianza vyema kuitumikia Real Madrid baada ya kuifungia bao moja ilipopata ushindi wa 2-0 dhidi ya Atalanta kwa Uwanja wa Warsaw Poland.


Huu ulikuwa mchezo wa Super Cup ukiwa wa kwanza kwa Mbappe tangu alipojiunga na Madrid kwenye dirisha hili la usajili alitokea PSG ya Ufaransa.


Umekuwa mwanzo mzuri kwa staa huyo baada ya kuifanikisha timu yake kutwaa ubingwa wa Super Cup na kuendelea kuweka rekodi.


Madrid ilianza kujipatia bao kupitia kwa staa wao Federico Valverde katika dakika ya 59 huku Mbappe akifunga dakika ya 68.


Hili linakuwa taji la kwanza la Super Cup kwa Mbappe ambaye alikaa PSG kwa miaka saba bila kutwaa taji hilo.


Staa huyo ambaye alicheza kama mshambuliaji wa mwisho alifanikiwa kuonyesha kombinesheni nzuri akisaidiana na Jude Bellingham na Vinicius Junior ambao walionyesha kiwango cha hali ya juu uwanjani.


Kwa matokeo hayo Mbappe ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kuifungia Madrid kwenye mchezo wake wa kwanza baada ya kusajili tangu Bellingham alipofanya hivyo Agosti 2023.


Madrid imeweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Super Cup mara sita.


Akizungumza kuhusu ushindi huo, Mbappe amesema kuwa anafurahishwa na jinsi alivyopata ushirikiano kutoka kwa mastaa wenzake wa Madrid.


“Sisi ni Real Madrid na hatuna kizuizi chochote, kama nitafunga mabao 50 basi elewa kuwa ni 50 jambo la msingi zaidi kwangu ni timu kushinda na kutwaa makombe.


“Huu ni usiku bora sana kwangu. Nimekuwa nikisubiri sana usiku huu, kucheza nikiwa ni nimevaa jezi ya Madrid ni kitu kizuri sana. Ni siku nzuri sana kwangu.


“Kutwaa ubingwa ni jambo zuri na nafahamu kuwa Madrid itaendelea kufanya vizuri na kutwaa makombe mengi zaidi,” alisema Mbappe.


Kocha wa rekodi kwenye kikosi cha Madrid Carlo Ancelotti, alisema kuwa Mbappe ni mchezaji muhimu zaidi kwenye kikosi chake.


“Mbappe ana uwezo wa juu wa kufunga mabao, lazima tuangalie balansi ya timu jinsi inavyotakiwa kucheza.


“Nafikiri leo tumeona kipindi cha kwanza jinsi tulivyocheza, bado tunaweza kucheza vizuri kama tutajidhatiti na kucheza kwa kiwango chetu.


“Tulipata shida kipindi cha kwanza, kwa kuwa Atalanta walikuwa bora sana kwenye eneo la kujilinda, walifanikiwa kuzuia mashambulizi yetu mengi, lakini kipindi cha pili tulirudi na kuwa bora zaidi,” alisema kocha huyo aliyeipa Madrid ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.


Mchezo huo pia ulimshuhudia kiungo mkongwe Luka Modrić akiweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Madrid kutwaa makombe mengi zaidi baada ya kufikisha 27, akiwa ni zaidi ya wengine wote.


Timu ya pili kwa kutwaa ubingwa huo mara nyingi ni Barcelona ambayo imetwaa mara tano, AC Milan nayo imetwaa mara tano huku Liverpool ikitwaa mara nne.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad