Jaji Wilson Dyansobera kutoka Mahakama kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam amesema baada ya Mahakama kusikiliza hoja za pande zote mbili na kupitia kwa makini kiapo cha mwombaji aitwaye Mohammed H. Zimu ambaye ni rafiki wa karibu wa Deusdedith Soka na wenzake wawili (2) imejiridhisha kwamba waombaji hawapo chini ya Jeshi la Polisi.
Akitoa maamuzi hayo leo, Jumatano Agosti 28.2024 Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam Jaji Dyansobera amesema, "hakuna malezo yanayotoka kwa muombaji kwamba alishuhdia waombaji wakiwa wanashikiliwa na Polisi au kuwa kizuizini.”
Katika maelezo yake Jaji Dyansobera ameeleza kuwa inawezekana muapaji alishuhudia wakikamatwa lakini hakuna ushahidi ya kuwa Soka na wenzake wapo kizuizini (detained) au wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kituo cha Chang’ombe, Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Jaji Dyansobera ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kufanya uchunguzi ili kufahamu walipo Soka pamoja na wenzake huku akisisitiza ni wajibu kwa Jeshi hilo, pia ni matakwa ya sheria za Kimataifa kwa chombo hicho cha usalama kufuatilia na kufahamu wako wapi raia ambao wamepotea.
"Mahakama inatoa amri kwa Polisi hasa mjibu maombi wa kwanza, mjibu maombi wa pili, mjibu maombi watatu, mjibu maombi wanne, na mjibu maombi watano kuchunguza uwepo wa hawa waombaji wako wapi” amesema Jaji Dyansobera.
Hata hivyo Jaji huyo amesema waleta maombi wana nafasi ya kukata rufaa juu ya kesi hiyo.