Max Nzengeli Aidhibu Simba Kimoko, Simba washindwa Kurudisha



YANGA wameendeleza ubabe wao kwa Simba baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mchezo huo uliokuwa na amshaamsha nyingi mwanzo hadi mwisho, Maxi Nzengeli ndiye aliyepeleka kilio Msimbazi kwa bao lake dakika ya 44 kipindi cha kwanza.

Mchezo ulianza kwa kasi kukiwa na mashambulizi ya hapa na pale ambapo Simba walikuwa wa kwanza kulishambulia lango la Yanga baada ya Shomari Kapombe kupiga krosi dakika ya kwanza lakini wenzake wakashindwa kuitumia vizuri Djigui Diarra akadaka.

Yanga walilipa shambulizi hilo dakika ya tatu baada ya Prince Dube kupokea pasi nzuri kutoka kwa Pacome Zouzoua, akachagua engo nzuri ya kuupeleka mpira ukampita kipa wa Simba, Moussa Camara lakini ukaishia kugonga nguzo ya pembeni kwa chini na kurudi uwanjani, Simba wakaokoa.



Hadi inafika dakika ya 15 tangu kuanza kwa mchezo huo, Simba ilikuwa imefanya mashambulizi matatu na Yanga mawili.

Mchezo ulitawaliwa na kasi huku kila timu ikionekana kupokonya mpira ndani ya muda mfupi baada ya kuupoteza jambo lililofanya kutokuwepo timu iliyofikisha angalau pasi kumi kwa wakati mmoja kabla ya mpinzani kumpokonya.

Yanga walikuwa na furaha zaidi kipindi cha kwanza baada ya Maxi Nzengeli kuwapa bao la uongozi dakika ya 44 akimalizia pasi nzuri ya Pacome Zouzoua baada ya kupigwa ‘one two’ za maana na nyota wa kikosi hicho.

Hilo ni bao la tatu Maxi anaifunga Simba tangu alipoanza kukutana nayo msimu uliopita ambapo mawili aliyafunga katika ushindi wa 5-1.

Dakika 45 za kwanza, kulikuwa na faulo nyingi zilizofanyika zikifika 14 kila upande ukiwa nazo saba ambapo Deborah Fernandes akiongoza kwa kuwa nazo tatu wakati Khalid Aucho akifanya mbili na kuwa kinara wa Yanga.

Ilishuhudiwa makocha wa timu zote mbili, Miguel Gamondi wa Yanga na Fadlu Davids wa Simba wakisimama muda wote wa dakika 45 za kwanza wakitoa maelekezo ya hapa na pale kwa wachezaji wao na kuacha viti wazi ikionekana ni vya moto kwao. Waliporudi kipindi cha pili Fadlu alivua koti la suti alilovaa kipindi cha kwanza na kubaki na shati wakati Gamondi akiendelea na muonekano wake wa mwanzo akiwa na t-shirt na track suit.

Kipindi cha pili wakati kinaanza, Yanga walifanya mabadiliko kwa kumtoa Prince Dube nafasi yake ikachukuliwa na Clement Mzize wakati Simba nao walimtoa Mzamiru Yassin akaingia Augustine Okejepha.


Gamondi katika kuendelea kulinda uongozi wa bao lake, dakika ya 63 akaamua kumtoa kiungo mshambuliaji, Duke Abuya akampa nafasi kiungo mkabaji, Mudathir Yahya ambaye pia ana uwezo wa kucheza kiungo mshambuliaji.

Fadlu kila alipokuwa akiangalia muda anaona hakuna dalili ya bao, dakika ya 70 akawaingiza mchezoni Kibu Denis na Fabrice Ngoma akawatoa Steven Mukwala na Deborah Fernandes.

Haikuishia hapo, dakika ya 75 akatoka Shomari Kapombe na Edwin Balua akaingia Kelvin Kijili na Freddy Koublan.

Clatous Chama aliingia kupambana na waajiri wake wa zamani Simba dakika ya 77 akichukua nafasi ya Stephane Aziz Ki.

Yanga walifanya tena mabadiliko dakika ya 88 alitoka Pacome na Maxi akaingia Kennedy Musonda na Bakari Mwamnyeto.

Mchezo huo ulitawaliwa na mastaa wa kigeni zaidi kutokana na kuwa na idadi kubwa ambapo kati ya nyota 22 wa pande zote mbili, wazawa walikuwa sita pekee, wawili wakiwa manahodha. Dickson Job (Yanga) na Mohamed Hussein (Simba).


Yanga walianza na kikosi kilichokuwa na wazawa wakiwa wawili pekee ambao ni Ibrahim Bacca na Dickson Job. Kikosi kamili kilikuwa hivi; Djigui Diarra, Yao Kouassi, Chadrack Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Duke Abuya, Prince Dube, Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua.

Kwa upande wa Simba walianza na wazawa wanne, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Mzamiru Yassin na Edwin Balua. Wakimataifa saba.

Kikosi chao kilianza hivi; Moussa Camara, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Chamou Karaboue, Che Malone Fondoh, Deborah Fernandes, Edwin Balua, Mzamiru Yassin, Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua na Joshua Mutale.

Simba wamepoteza mchezo wa tatu mfululizo dhidi ya Yanga baada ya msimu uliopita kwenye ligi kufungwa 5-1 na 2-1. Lakini pia hii ni mara ya tatu mfululizo Simba inafungwa na Yanga katika Ngao ya Jamii iliyochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa baaa ya mwaka 2021 matokeo kuwa 1-0 na 2022 kuwa 2-1.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad