Klabu ya Simba imefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kuvunja mkataba na aliyekuwa mshambuliaji wake Freddy Michael Koublan ambaye hakukidhi mahitaji ya kocha Fadlu Davies.
Simba imefikia hatua hiyo baada ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji, Leonel Ateba kutoka USM Alger. Baada ya kuachwa na Simba Freddy Michael ametua Katika Klabu ya USM Alger ambapo Leonel Ateba ametokea.
Akizungumzia hilo, mchambuzi wa masuala ya soka nchini kutoka Wasafi Media, George Job amesema; “Simba wamekurupuka kuachana na Freddy Michael. Huu ni uamuzi wa kushangaza. Unamuachaje mtu aliyefunga mabao 7 Ligi ya Tanzania na mabao 14 Zambia kisha unamsajili mshambuliaji aliyefunga bao moja, inashangaza. Wangemtoa Fredd kwa ajili ya mtu ambaye amekuja akiwa top scorer ningeelewa.
“Freddy alijitetea kwa namba, alifaa kuwa hata chaguo la pili katika benchi kuliko kuachana nae kabisa. Yawezekana akawa sio level ya Simba, kumuongezea watu ilikuwa sahihi, angeachwa agombanie namba hata mpaka dirisha dogo, lakini kumtoa kwa sababu umeleta mtu ambaye namba zake hazifiki hata robo ya Freddy, hii inashangaza.
“Itakuwaje iwapo huyu mshambuliaji mpya (Ateba) akishindwa kufikia malengo ambayo Simba walitarajia, watakuwa wamefanya kosa lile lile mara mbili mfululizo, waliwatoa Baleke na Phiri hivi hivi wakaleta Jobe na Fredd, kwenye hili viongozi hawawezi kukwepa lawama. Nina wasiwasi mkubwa na kiwango cha Ateba,” amesema George Job.