Chidimma Adetshina ameamua kujitoa kwenye shindano la Miss Afrika Kusini 2024, siku chache baada ya kuwa gumzo nchini humo kwa kudaiwa kwamba si raia wa Afrika Kusini na kutakiwa kujiondoa.
Katika taarifa aliyoitoa kupitia akaunti yake rasmi ya Instagram, Adetshina mwenye umri wa miaka 23 alishukuru watu wake kwa kumuunga mkono na kueleza kwamba uamuzi wake umetokana na kutaka usalama na ustawi wa familia yake.
Adetshina, ambaye ni mzaliwa wa Soweto, Afrika Kusini, na baba Mnaijeria na mama Mmozambique, aliingia kwenye Top 30 ya mashindano hayo. Hata hivyo, alikumbana na mjadala mkali kuhusu uraia wake baada ya Idara ya Mambo ya Ndani kugundua udanganyifu uliofanywa na mama yake. Waziri wa Idara ya Mambo ya Ndani, Leon Schreiber, alithibitisha.
Kutokana na hali hiyo, Adetshina amechukua uamuzi wa kujiondoa kutoka kwenye mashindano hayo, akisisitiza kwamba amekuwa sehemu ya safari ya kuvutia lakini ameamua kujali usalama na ustawi wa familia yake na yeye mwenyewe.
"Kuwa sehemu ya shindano la Miss Afrika Kusini 2024 imekuwa safari ya kuvutia sana, hata hivyo, baada ya kutafakari kwa kina, nimechukua uamuzi mgumu wa kujiondoa katika mashindano hayo kwa ajili ya usalama na ustawi wa familia yangu na mimi mwenyewe."