Muunganiko wa DUBE na Mudathiri Wamfungua Macho KOCHA Gamondi.....

 

Muunganiko wa DUBE na Mudathiri Wamfungua Macho KOCHA Gamondi.....

Ni kama straika Prince Dube amemfungulia ‘code’ kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ya namna ya kumfanya aendelee kucheka na nyavu ndani ya kikosi hicho baada ya staa huyo kutamka kwamba muunganiko alionao akicheza na Mudathir Yahya una kitu kikubwa kitakachoibeba timu hiyo msimu huu.


Dube aliyejiunga na Yanga msimu huu baada ya kuachana na Azam, amefichua siri kuwa mtu anayefahamu vizuri zaidi mikimbio yake ndani ya uwanja ni Mudathir kutokana na wawili hao kucheza pamoja kwa kipindi cha misimu miwili walipokuwa Azam kabla ya sasa kukutana tena Yanga.


Kauli ya Dube inaendana na kile wawili hao walichofanya dhidi ya waajiri wao wa zamani, Azam FC katika mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii uliochezwa Agosti 11, 2024 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.


Dube na Mudathir ambao walicheza pamoja ndani ya Azam kwa misimu miwili 2020-2021 na 2021-2022, wamekutana tena ndani ya Yanga msimu huu baada ya kila mmoja kuondoka viunga vya Azam Complex kwa nyakati tofauti.


Alianza Mudathir kusajiliwa na Yanga Januari 2023 akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Azam kumalizika mwishoni mwa msimu wa 2021-2022, kisha akafuata Dube msimu huu 2024-2025 akiondoka Azam baada ya kuvunja mkataba.


Baada ya mchezo wa Jumapili iliyopita ambao Dube alifunga bao la kusawazisha kwa Yanga waliposhinda 4-1 dhidi ya Azam akimalizia pasi ya Mudathir, straika huyo alisema: “Mikimbio yangu Mudathir anaijua vizuri kwani hata tukiwa Azam nilikuwa nafunga kama hivi. Kwa hiyo muunganiko uleule umerudi tena.”


Aina ya bao alilofunga Dube na pasi aliyopokea kutoka kwa Mudathir, imewakumbusha nyota hao na mashabiki wa soka kwa ujumla kilichotokea Oktoba 15, 2020 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam wakati Azam ikiichapa Mwadui mabao 3-0 ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.


Katika mchezo huo, dakika ya 60, Mudathir alipiga pasi ndefu iliyomfikia Dube ambaye alimchambua kipa akafunga. Unaweza kusema Jumapili iliyopita ilikuwa ni kama marudio ya bao hilo lakini safari hii wachezaji hao wakiwa na jezi ya Yanga dhidi ya timu yao ya zamani ya Azam ambapo dakika ya 19, Dube tena anapokea pasi ndefu kutoka kwa Mudathir, anamchambua kipa na kufunga likiwa ni bao la kusawazisha, mwisho Yanga ikashinda 4-1.


Ukiachana na bao hilo, Dube katika misimu miwili akicheza sambamba na Mudathir ndani ya Azam, alinufaika na pasi tano kutoka kwa kiungo huyo kati ya mabao 15 aliyofunga ya ligi wakiwa pamoja.


Msimu wa 2020-2021 ambao ulikuwa wa kwanza kwa Dube kuitumikia Azam akitokea Highlanders ya kwao Zimbabwe, alimaliza ligi akifunga mabao 14, huku manne kati ya hayo yakitokana na pasi za mwisho za Mudathir.


Mechi hizo ni; Azam 3-0 Mwadui (Oktoba 15, 2020), Kagera 1-2 Azam (Machi 3, 2021), Azam 2-0 Mtibwa (Aprili 9, 2021) na Azam 2-1 KMC (Mei 15, 2021).


Baada ya hapo, msimu wa 2021-2022 ambao Dube alifunga bao moja katika ligi kutokana na kuwa nje ya uwanja muda mrefu akiuguza majeraha, Mudathir alihusika kwa namna moja ama nyingine katika bao hilo kwani pasi yake ilikwenda kwa Rodgers Kola kabla ya kumfikia mfungaji Dube.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad