Nyuma ya Pazia Matumizi ya Sawa za P2 na Misoprostol



Dar es Salaam. Kama wewe ni mtumiaji wa dawa za dharura za kuzuia ujauzito 'Emergence Contraceptive Pills' vidonge maarufu kama P2 au dawa zinazotumiwa ndivyo sivyo na wengi kutolea mimba misoprostol, huenda kuna mengi usiyoyajua kuhusu matumizi sahihi na zaidi ya dawa hizo.

Wataalamu wa afya wamebainisha kuwa dawa hizo tofauti na zinavyotumiwa ndivyo sivyo na watumiaji wengi, zimetengenezwa kwa ajili ya kutibu changamoto mbalimbali zinazohusiana na afya ya uzazi kwa mwanamke na zina viwango tofauti katika utumiaji.

Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama kutoka Hospitali ya misheni Ifakara, mkoani Morogoro, Elias Kweyamba anasema dawa za misoprostol ukitumia kwa lengo ambalo limetarajiwa hutoa matokeo chanya.

“Kuna watu wanatumia tofauti na maelekezo kwa kutaka kupata kitu tofauti, matumizi ya miso yanahusisha kupunguza utokaji damu baada ya mama kujifungua au kumsaidia mama aliyetokwa damu nyingi au amejifungua kama tiba ya kuzuia kuvuja damu,” anasema.

Anasema pia hutumika kwa mimba ambayo imepitiliza miezi tisa bila mhusika kujifungua, hivyo anawekewa ili kuimarisha uchungu kwa mjamzito anayesaidiwa kujifungua au kwa ambaye mtoto amefia tumboni.

Pia Dk Kweyamba anasema miso hutumika kusafisha kizazi ambacho mimba imeharibika kwa sababu zozote zile kwa kutolewa au kutoka yenyewe.

“Pamoja na mifano hii ya moja kwa moja, ila matumizi yanatofautiana kulingana na hali ya mgonjwa na mtabibu atakavyoona inafaa, hivyo ni muhimu kuzitumia kwa ushauri wa daktari na si vinginevyo.”

Hata hivyo, wataalamu wanasema miso haishauriwi kutumika kama njia za utoaji mimba mpaka pale daktari awe amemwandikia mgonjwa, kama anavyosema Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi, Ali Said.


“Wanaotumia dawa za kutoa mimba maarufu miso, wamekuwa wakikutana na changamoto ya kushindwa kukadiria umri wa mimba na vidonge vingapi atumie, hivyo wengi wanatoa mimba lakini haitoki kikamilifu na wengine kuvuja damu nyingi,” anasema Dk Said, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo cha Sayansi na Afya Shirikishi (Muhas).

Kuhusu P2, Dk Kweyamba anasema kuwa inatumika kama njia za uzazi wa mpango na hutumika kwenye dharura kwa ajili ya kuzuia mimba.

“Kwa mfano mtoto amebakwa, kama mtu alikuwa anatumia dawa za uzazi wa mpango amesahau, kondomu imepasuka au amefanya tendo pasipo kutarajia na kakuta siku zake amekosea kuhesabu.


“Kazi yake kuzuia na si kutoa kwa kuwa ni njia ya dharura, ina kiwango kikubwa cha kichocheo, akiitumia tofauti na maelekezo ya wataalamu kwa maana ya dharura, mhusika anaweza kupata changamoto ya kupata ujauzito huko mbeleni, sababu ina kichocheo ambacho kikiwa kingi mwilini kinasababisha madhara,” anasema.

Dk Kweyamba anasisitiza kuwa huzuia mimba kuwepo na inatumika ndani ya saa 72 toka tendo limetokea na si zaidi ya hapo.

Mtaalamu wa afya ya uzazi kwa vijana na Mkuu wa Programu kutoka Youth Choice For Change (YCC), Godlove Isdory anasema kitaalamu hushauriwa katika kipindi cha ndani ya miezi 12 mwanamke angalau ameze mara tatu kwa sababu kiambata chake ni kama dawa za uzazi wa mpango, hivyo zikiwa nyingi zinaweza kuvuruga homoni.

Anasema P2 mbili zina vichocheo vikali ambapo ukitumia ni sawa na mtu aliyekunywa vidonge 60 vya majira,” anasema Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi, Living Colman.

Uviaji mimba

Dk Said anasema utafiti uliofanyika mwaka 2018 ulionyesha mimba takribani milioni 2.9 hutungwa kila mwaka.

"Miongoni mwa hizo, utafiti ulionyesha mimba milioni 1.3 hazikupangwa, mimba 430,000 hutoka au kutolewa na vifo vitokanavyo na utoaji mimba usio salama ni asilimia 19," anasema Dk Said.

Ingawaje mimba zinazoharibiwa ambazo hurekodiwa ni 430,000 kwa mwaka, wataalamu hao wamesema idadi ni kubwa zaidi, kwani wanaofika vituoni kuhitaji msaada wa kitabibu, ni wale waliopata madhara ya papo kwa papo baada ya kutoa mimba.

Mkurugenzi wa Kanda wa Mtandao wa kimataifa wa wanawake wa haki za uzazi Afrika (WGNRR AFRICA), Nondo Ejano anasema utoaji mimba usio salama unachangia hadi asilimia 19 ya vifo vya uzazi nchini Tanzania, huku huduma ya afya kwa ajili ya kudhibiti matatizo ya utoaji mimba usio salama inagharimu mfumo wa afya wa Serikali Sh10.4 bilioni kwa mwaka.

“Gharama hizi za kibinadamu na za kifedha zinaweza kuepukika kwa kiasi kikubwa na hii inaweza kutoa rasilimali kutumika mahali pengine, ikiwa sheria zitafanyiwa marekebisho,” anasema Ejano.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad