Jeshi la Polisi limesema liliwakamata Viongozi na Wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wapatao 520 wakiwemo Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Bara Tundu Lissu, Katibu Mkuu Mnyika na wengine waliotaka kushiriki kongamano la Vijana Jijini Mbeya lililopigwa marufuku na Polisi ambapo wamesema kwa sasa Viongozi hao na Wafuasi wa CHADEMA wamesafirishwa kwa escort na kurudishwa Mikoa wanayotoka na kuachiwa huru huku baadhi yao wakiachiwa kwa dhamana.
Akiongea usiku wa kuamkia leo August 13,2024 Jijini Mbeya, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo Nchini, Awadhi Haji amesema August 11,2024 walikamatwa Watu 375 wakiwemo Wanaume 261 na Wanawake 114 na August 12,2024 wamewakamata Watu 145 wakiwemo Wanaume 112 na Wanawake 33 ambapo pia wamekamata magari 25.
Mwandishi wa @AyoTV_, Bakari Chijumba amemuuliza Kamanda Awadhi kuhusu hatima ya Viongozi waliosafirishwa na kuhusu taarifa za Lissu kutopewa dawa zake akiwa ameshikiliwa ambapo ametoa majibu kuhusu hilo huku pia akikiri kuwa wote wamerudishwa walikotokea na kwamba ambao hawakuachiwa ni walioshindwa kukidhi masharti ya dhamana au kuwa na makosa zaidi ya moja, ikiwemo jinai.