Polisi Waeleza Kifo Cha Msanii Man Dojo..




JESHI la Polisi mkoani Dodoma, limetaja sababu za kifo cha msanii wa nyimbo za Bongo Fleva, Joseph Francis maarufu Mandojo, kuwa ni kukutwa kwenye kibanda cha mlinzi ambaye aliita mwizi na watu kujitokeza na kumshambulia.

Mandojo anadaiwa kuuawa kwa kupigwa na watu wasiojulikana kwa kutuhumiwa kuwa ni mwizi katika uzio wa Kanisa Katoliki eneo la Nzuguni B, jijini Dodoma.

Aidha, taarifa kutoka eneo hilo zinadai kuwa msanii huyo alikwenda kanisani hapo kwa ajili ya kusali.

Akizungumza na Nipashe, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Anania Amo, alisema Mandojo alikutwa na mlinzi wa eneo hilo majira ya saa 10:00 alfajiri ndani ya kibanda chake.

Alisema baada ya mlinzi kuona hivyo, alipiga kelele kisha watu waliokuwapo eneo hilo na wengine wanaodhaniwa kuwa ni waamini wa kanisa hilo waliokuwa kanisani, walimshambulia kwa kumpiga hadi kufariki dunia.

"Mandojo alituhumiwa mwizi, mlinzi alipopiga kelele kwa muda ule watu walijitokeza na kuanza kumshambulia kwa kipigo kilichosababisha umauti kumkuta, baada ya kubainika amefariki dunia mwili wake ulipelekwa katika Hospitali ya Rufani Dodoma," alisema Kaimu Kamanda Amo.

Hata hivyo, alisema ni kosa kisheria watu kujichukukia sheria mkononi.

“Ni vyema wangemkamata na kumpeleka katika kituo cha polisi kilichoko eneo la karibu, sio kujichukulia hatua mkononi kama walivyofanya,” alisema kamanda huyo.


Mtu wa karibu na Mandojo, aliyezungumza na mwandishi wa habari hii kwa sharti la kutotajwa jina, alisema msanii huyo alikwenda kanisani humo kwa ajili ya kusali na kuomba toba kutokana na ugomvi uliokuwa baina yake na mkewe.

Alisema lengo la Mandojo halikutimia na matokeo yake alikutwa na mauti, na kuzima ndoto na mipango yake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad