Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi amesema unywaji juisi iliyokamuliwa kwa matunda halisi, unaweza kuwa hatari kiafya kutokana na kiwango cha matunda kinachotumika kuwa kwa wingi.
Anasema kiafya tunda linapaswa kuliwa kama lilivyo kabla ya kulichakata ama kulikamua na kuwa juisi. Anasema kula matunda badala ya juisi kunasaidia mlaji kubaini kiwango na idadi ya matunda aliyokula.
Prof. Janabi, ambaye pia ni Mhadhiri Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Magonjwa ya Moyo cha Marekani (FACC), anatoa 'darasa' hilo katika kitabu chake cha 'Mtindo wa Maisha na Afya Yako'.
"Ni vyema kula tunda lilivyo kuliko kukamua juisi. Kwa mfano, ili upate glasi moja ya juisi ya chungwa, unahitaji machungwa matano.
"Ukinywa glasi tatu kwa siku, yaani asubuhi, mchana na jioni, maana yake itakuwa umekula machungwa 15 na kwa siku 10 ni sawa machungwa 150 na kwa mwezi ni machungwa 450.
"Hicho ni kiasi kikubwa sana ambacho kinaweza kuleta shida mwilini kutokana na kiwango chake cha sukari," anasema Prof. Janabi ambaye pia ni bingwa wa magonjwa ya moyo.
Anasema tatizo la magonjwa yasiyoambukiza (NCD), ni janga na chimbuko lake ni tabia ya ulaji chakula usio sahihi.
"Kwa maana hiyo, njia ya kwanza kushughulika na janga hili ni kuzingatia mwenendo unaofaa wa ulaji chakula. Jamii inapaswa kula chakula kwa usahihi wake," anasema.