Rais Samia Afunguka Sababu ya Kumuita Simba 'Tundu Lissu

 

Rais Samia Afunguka Sababu ya Kumuita Simba 'Tundu Lissu

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwahutubia viongozi, wageni mbalimbali pamoja na wananchi wakati wa kilele cha Tamasha la Kizimkazi katika uwanja wa Mwehe, Kusini Unguja, Zanzibar tarehe leo Agosti  25, 2024.


Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan ametaja sababu za kutaka simba aitwe jina la Tundu Lissu, makamu mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).


Amesema aliamua hiyo kutokana na umachachari na ukorofi wa mwanasiasa huyo. Rais Samia ametoa kauli  hiyobAgosti 25, 2024 wakati akifunga Tamasha la Kizimkazi katika viwanja vya Mwehe, Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja. Ufafanuzi huo umetokana na kauli aliyoitoa jana alipotembelea maonyesho yaliyohusisha wanyamapori.


“Nataka niseme, jana kulikuwa kuna vijiclip vinarushwa, kulikuwa kuna simba machachari pale, mkorofi kidogo. Nikauliza, huyu simba mmempa jina? nikaambiwa bado, nikawaambia muiteni Tundu Lissu, mpeni jina lake huyu simba, kwa sababu alikuwa hatulii kama alivyo mwanangu Tundu Lissu," amesema Rais Samia.


Kufuatia tukio hilo, Mwananchi imezungumza Lissu akasema Rais Samia hajakosema kutokana na asili yake. Amesema yeye amezaliwa kwenye ukoo wa mashujaa wa Kinyaturu, watu waliowahi kuua simba wala ng'ombe na wezi wa ng'ombe wao.


“Kwa Kinyaturu mashujaa hao huitwa 'ahomi' (umoja 'muhomi'). Babu yangu mzaa baba, Mughwai, alikuwa muhomi; aliua simba aliyevamia na kuua ng'ombe wake.


Baba yangu aliyenizaa, Mzee Lissu naye alikuwa muhomi. Aliua simba mara mbili waliovamia na kuua ng'ombe wake,” amesema Lissu. Hivyo, amesema ijapokuwa Rais Samia anaweza asiyajue hayo, lakini hajakosea kumuita simba, mnyama anayehusishwa na nguvu, ujasiri na mamlaka katika tamaduni nyingi za dunia.


Suala hilo, mbali na wawili hao kulizungumzia, limeibua mijadala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii ikimuhusisha Lissu na ukosoaji wa mara kwa mara wa Serikali. Tamasha lakua zaidi


Wakati huohuo; Rais Samia amesema kutokana na kuendelea kukua kwa Tamasha la Kizimkazi, wameamua kuanzisha taasisi maalumu itakayolisimamia na kuliendesha kwa miaka ijayo.


Hivyo, ameitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha tamasha la hilo linatambulika rasmi ndani ya Serikali na liandaliwe kama matamasha mengine yanavyoandaliwa nchini.


Rais Samia amesema tamasha hilo linaendelea kukua kila mwaka na sasa linatumika kuendeleza mila, desturi na kuchangia kuchochea maendeleo, sio tu kwa mkoa linakofanyika bali kwa Taifa  zima.


“Kutokana na kukua kwa tamasha hilo, tumeamua kuanzisha taasisi maalumu ltakayosimamia na kuendesha tamasha hilo. Niombe Serikali ya Mapinduzi liandaliwe kama matamasha mengine,” amesema Samia.


Amesema tamasha hilo lililoanza kama sherehe za kijiji limekua kwa kiasi kikubwa na kwa sasa linatumika kuzindua miradi mikubwa ya maendeleo. Tamasha hilo ambalo mwaka huu lilizinduliwa Agosti 18, 2024 na Rais Hussein Mwinyi, limetumika kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi na shughuli mbalimbali za kijamiii na kiuchumi. 


Mbali na hilo, yametolewa mafunzo kwa wajasiriamali 605 wa fani za uvuvi, kilimo utalii na Sanaa, hivyo watakuza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.


Vilevile, kwenye tamasha hilo wamezindua uwanja wa michezo wa Suluhu Academy, ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 20,000 na kuagiza uwanja huo ukamilike Januari ili Februari 2025 michezo ianze kuchezwa katika uwanja huo. Uwanja huo utakuwa na michezo mbalimbali kama soka, riadha katika viwango vya kimataifa.


Akizungumzia mradi wa ufugaji wa kasa aliouzindua juzi Kizimkazi Dimbani, Rais Samia amesema si tu utasaidia kufungua uchumi, pia unaenda sambamba na malengo ya Serikali ya kuwahifadhi wanyama hao ambao wapo hatarini kutoweka. “Kama nilivyosema tamasha la mwaka huu lilikuwa la kipekee na mambo mengi yamefanywa,” amesema.


Amesema moja ya shughuli zilizofanywa na viongozi wakuu wa kitaifa, ni mdahalo wa nishati safi ulioongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, ili kuhakikisha nishati inayotumika inaendelea kuwa safi. Amesema katika mdahalo huo pia iligawiwa mitungi 1,500 ya gesi kuhakikisha wananchi wanaoondokana na matumzi ya kuni na mkaa.


Akizungungumzia kaulimbiu zilizotumika katika tamasha hilo mwaka jana na mwaka huu, Rais Samia amesema zimeakisi malengo ya Taifa.


“Mwaka jana kaulimbiu ilisema tuwalinde watoto wetu kwa masilahi ya Taifa, kwa hiyo ukiangalia miradi iliyotekelezwa zikiwemo ujenzi wa shule, viwanja vya michezo na vya kufurahishia watoto, vimeendana kaulimbiu hiyo,” amesema.  Amesema kuwepo kwa shule na viwanja mbalimbali kutaleta si tu burudani, bali pia vitawasaidia watoto kiafya na kiakili.


Ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa Kizimkazi kujipongeza kwa maendeleo hayo kwani yanakwenda kujibu hoja na kaulimbiu ya ulinzi wa mtoto. Kuhusu kaulimbiu ya mwaka huu isemayo ‘Kizimkazi imeitika’, Rais Samia amesema wameshuhudia kwamba kweli imeitika kwa ushiriki mzuri wa wadau waliokwenda na miradi ya maendeleo wakati wa tamasha.


“Imeitika kuunga juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuchangia miradi ya kijamii na kiuchumi na kupokea miradi ya uwekezaji, hatimaye kuchangia uchumi wa nchi yetu,” amesema.


Amewataka viongozi wa Mkoa na Wilaya kufuatilia utekelezaji wa miradi na mambo yote yaliyolengwa kufanyika kukuza uchumi wa nchi na kwamba mwakani wakiwa kwenye tamasha, lingine wapokee taarifa nyingine za maendeleo nzuri kama hiyo. Amewataka wananchi hao kuwa mstari wa mbele kuonyesha kuwa Kizimkazi imeitika kuhakikisha juhudi za wadau wote zinathaminiwa.


Katibu wa tamasha, Maalim Ahmed Said amesema tamasha hilo limesaidia kuboresha miundombinu mbalimbali na kiwango cha elimu katika ngazi ya msingi na sekondari. Amesema ufaulu kwa sekodari umepanda kutoka asilimia 71 hadi 85 mwaka 2022/23.


Awali mwenyekiti wa tamasha hilo, Mahfoudh Said Omar amesema tamasha hilo limekuwa na mafanikio makubwa kwani kuna shughuli mbalimbali za kiutamaduni, ufunguzi miradi ya maendeleo zimefanyika.


Tamasha hilo lilianza mwaka 2015 na ilikuwa ni sherehe ya kumuaga Samia Suluhu Hassan baada ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Rais John Magufuli. Baada ya kuteuliwa Samia alipokutana na wananchi wa Kizimkazi na kufanya sherehe ya kumuaga 2016 iliyojulikana Samia Day na ilipofika nwaka 2017 jina likabadilishwa na kuwa Kizimkazi Day.


Samia aliwaambiwa wananchi hao siku hiyo itakuwa siku maalumu ya kukutana kwa wakazi hao ili kujadili maendeleo yao. Kufikia mwaka 2020 ndipo likaanzishwa rasmi Tamasha la Kizimkazi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad