SIMBA ilimaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya tatu kwa kuvuna pointi 69, sawa na Azam FC waliomaliza katika nafasi ya pili, lakini Azam waliongoza kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.
Kwahiyo ni wazi kwamba leo ndio siku ya mashabiki na wadau wa klabu hiyo kutembea kibabe sana kwenda kwenye mtoko matata kabisa wa Simba Day. Wanatesti mitambo dhidi ya APR ya Rwanda.
Ndani ya vaibu hilo wapo wachezaji ambao watatangazwa kwa mara ya kwanza na wengine ni wakongwe;
Simba Day 2024... Ni shoo ya King Kiba
WAKONGWE
MOHAMED HUSSEIN
Ni miongoni mwa wachezaji wakongwe na wazawa walioitumikia Simba kwa kipindi kirefu, Tshabalala yupo Simba kwa msimu wa 11 sasa kwani alitua Msimbazi mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar.
Beki huyo wa kushoto wa Simba tangu atue ndani ya kikosi hicho, hajawahi kupata mbadala wake wa kumpokonya namba, licha ya makocha zaidi ya 10 kufundisha timu hiyo. Alikalishwa benchi kwa muda mfupi sana na Asante Kwasi pekee na hakuna mwingine sio mzawa wala mgeni aliyeweza kumng’oa.
Amebeba mataji manne ya Ligi Kuu Bara tangu, 2017-18, 2018-19, 2019-20 na 2020-21, kwa upande wa Kombe la FA nako amechukua manne, 2016-17, 2019-20, 2020-21 na 2023-24 huku Simba ikiwa na rekodi ya kuyabeba sita.
SHOMARI KAPOMBE
Mkongwe mwenye miaka 32 akitokea Morogoro, ni mchezaji wa muda mrefu Simba akiitumikia kwa misimu tangu alipotua 2017 akitokea Azam FC.
Amekuwa beki kisiki kwani muda mwingi amekuwa akipangwa katika kikosi cha kwanza, huku akiwakalisha wachezaji waliosajiliwa nafasi moja na yeye kutokana na kiwango chake kuwa bora.
Hii ni Simba Day yake ya nane.
Ana rekodi kubwa ya uzoefu wa kucheza michuano ya kimataifa na ligi, huku akiwa na mataji matatu ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho FA akiwa na rekodi hizo hizo.
Licha ya rekodi hizo, Kapombe ni beki ambaye anasifika kwa kuzuia na kupandisha mashambulizi, jambo lililomuongezea thamani zaidi ya kusalia ndani ya kikosi hicho.
AISHI MANULA
Ni mchezaji mwingine mkongwe ndani ya kikosi hicho japo kwa muda mrefu amekuwa nje ya uwanja kutokana na tatizo la kitabibu na hakuwa katika kambi ya timu hiyo jijini Ismailia, Misri.
Naye alitua Msimbazi mwaka 2017 akiwa na kina Erasto Nyoni na John Bocco ambao hawapo na timu hiyo kwa sasa, lakini ni kipa mwenye mafanikio makubwa kwa miaka ya hivi karibuni akiibeba Simba ndani na kimataifa kabla ya mambo kutibuka baada ya kipigo cha 5-1 kutoka kwa Yanga.
Hakuna anayejua kinachoendelea baina ya kipa huyo na mabosi wake, lakini kama hajatolewa kwa mkopo kama ilivyokuwa ikielezwa awali, basi naye atakuwepo tamashani kama kawaida kutambulishwa.
KIBU DENIS
Alijiunga na Simba 2021/2022 akitokea Mbeya City, ametumika ndani ya kikosi hicho misimu mitatu mfululizo, huku msimu ujao ukiwa ni wanne kwake. Amekuwa mzawa mwenye kiwango kizuri kilichomfanya kupewa nafasi na makocha waliowahi kupita katika timu hiyo kama Juma Mgunda, Robertinho Oliviera na Abdelhak Benchikha.
Wengi wanamkumbuka katika mchezo uliopita alipofunga bao la pekee katika dabi ya Simba na Yanga, licha ya wao kufungwa mabao 5-1, anasifika kwa wepesi wake anapokuwa uwanjani na jinsi anavyowapa tabu wapinzani.
Amebeba mataji mawili ya Ligi Kuu na mawili ya Kombe la Shirikisho.
Hata hivyo, jamaa hakuwepo kambini Misri kwani alienda Norway kutesti zali la kucheza soka la kulipwa na amesharejea kimyakimya baada ya mabosi wa klabu hiyo ya Msimbazi kuchomoa dau lililotakiwa kutolewa na klabu ya Kristiansund BK iliyokuwa ikimtaka kumsajili.
Kama mabosi wameamua kumalizana naye kimyakimya klabuni, basi jamaa naye atakuwepo tamashani na kuongeza idadi ya nyota watakaounda kikosi cha msimu ujao.
WAGENI
AUGUSTINE OKEJEPHA
Kiungo mshambuliaji wa Rivers United ya Nigeria, huu ndio msimu wake wa kwanza ndani ya kikosi cha Simba na hii itakuwa siku yake ya kwanza kucheza mechi ya kirafiki na APR ya Rwanda kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa akiwa amevalia jezi hiyo nyekundu.
Ana rekodi ya kuwa mfungaji bora wa ligi ya Nigeria msimu uliopita na katika nafasi yake ambayo hapo awali ilikuwa ikichezewa na Clatous Chama anacheza pamoja na Yusuf Kagoma kutoka Singida Black Stars na Debora Fernandes kutoka Mtondo ya Zambia.
Ndani ya kikosi cha Simba tayari ameshaonyesha makali yake, kwani alifunga bao katika dakika ya 120 ya mchezo dhidi ya Suez Canal ikiwa ni mechi ya kwanza ya kujipima nguvu Misri.
JEAN AHOUA
Kiungo Muivory Coast (22) ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili na Wekundu wa Msimbazi akitokea klabu ya Stella Club d’Adjame’ ya nchini humo, hii itakuwa Simba Day yake ya kwanza.
Katika msimu wa 2023/24, Ahoua ameibuka kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu nchini Ivory Coast (MVP) na klabu yake, huku akifunga mabao 12 na kutoa ‘asisti’ tisa. Kiungo mshambuliaji huyu anasifika kwa kufunga mabao mengi kutokea nje ya box, kuchezesha timu, pamoja na kutengeneza nafasi kwa wenzie.
Licha ya ugeni tayari mguu wake umeshaongea kwa kufunga mabao mawili ndani ya dakika mbili, la kwanza 14 na 16 katika mechi ya kujipima iliyochezwa kwa saa mbili huko Misri.
JOSHUA MUTALE
Joshua Mutale ni mmoja kati ya wachezaji mahiri ambao wametambulishwa kujiunga na klabu hiyo, ambayo kwa sasa ipo katika uboreshaji wa kikosi chake kuelekea msimu wa 2024/2025. Mutale ni mchezaji wa pili kutambulishwa baada ya Lawi ambaye hata hivyo ishu yake iliingia utata na hivi sasa yuko Ulaya.
Mutale, 22, ana uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani kwa ufanisi wa hali ya juu. Anaweza kumudu nafasi ya winga wa kulia, kushoto na wakati mwingine anacheza nyuma ya mshambuliaji, yaani namba 10. Akiwa na timu ya Power Dynamos msimu uliopita, Mutale alifunga mabao matano na kuisaidia timu yake kupata mengine matatu katika michezo 26.
STEVEN MUKWALA
Klabu ya Simba SC imemsajili Steven Mukwala kutoka Klabu ya Asante Kotoko ya nchini Ghana.
Mukwala alikuwa mchezaji wa tatu kutambulishwa Simba baada ya Lameck Lawi na Joshua Mutale.
DEBORA FERNANDES
Kiungo wa kati Debora Fernandes Mavambo kutoka Mutondo Stars ya Zambia amesaini mkataba wa miaka mitatu Msimbazi. Debora ambaye ana uraia pacha wa Congo Brazaville lakini anachezea timu ya taifa ya Gabon, anamudu pia kucheza kama kiungo mkabaji ingawa anapendelea zaidi kucheza kama kiungo wa kati (namba 8).
VALENTIN NOUMA
Beki wa kushoto wa timu ya taifa ya Burkina Faso na FC Lupopo, Valentin Nouma mwenye umri wa miaka 24 kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.
KARABOUE CHAMOU
Huyu ni mlinzi wa kati raia wa Ivory Coast kutoka klabu ya Racing Club d’ Abidjan na amesaini mkataba wa miaka miwili. Usajili wake unaongeza nguvu mpya kwenye safu ya ulinzi ya Simba, ambako imeondokewa na Henock Inonga na Kennedy Juma.
YUSUPH KAGOMA
Kiungo mkabaji Yusuph Kagoma ni miongoni mwa wachezaji wapya katika kikosi cha Simba SC, amesaini mkataba wa miaka mitatu akitokea Singida Fountain Gate. Msimu uliopita Kagoma alicheza mechi 18 akitumia dakika 1,373.
AWESU AWESU
Huu ni msimu wa kwanza kwake kuwa na Simba iliyomsajili kutoka KMC na ni mmoja ya viungo mahiri anayemudu kucheza kama mkabaji na ushambuliaji.
Naye anatarajiwa kuwasha moto tamashani mbele ya halaiki ya mashabiki wa Simba ambao wamejiandaa kupata burudani ya tamasha la 16 la Simba Day.