UONGOZI wa Simba umebainisha kuwa taratibu nyota wao wanazidi kuimarika kutokana na maandalizi mazuri ambayo wanayafanya chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids.
Simba mchezo wa kwanza wa ligi uliochezwa Uwanja wa KMC, Mwenge iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United mabao yakifungwa na Che Malone dakika ya 14, Valentino Mashaka dakika ya 64 na Awesu Awesu dakika ya 90.
Katika mchezo huo kiungo Awesu ambaye alianzia benchi alikuwa kwenye siku nzuri kazini kwenye mchezo wake wa kwanza wa ushindani akiwa na uzi wa Simba.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa wanatambua umuhimu wa kila mchezaji hivyo uwezo wa Awesu unatokana na ushirikiano kutoka kwa wachezaji wote.
“Timu inazidi kuimarika na unaona namna ambavyo kila mmoja anashirikiana na mwingine kwenye kutafuta matokeo, sio Awesu Awesu pekee bali Kibu Dennis, Valentino Mashaka, Aishi Manula wote ni wachezaji wa Simba na wanafanya kazi kwa ushirikiano, kazi bado inaendelea.
“Mashabiki tuzidi kuwa pamoja kwani kazi inaendelea na msimu huu malengo ni kupata ushindi kwenye mechi zetu na kuwapa furaha Wanasimba yaani Ubaya Ubwela.”