Simba Waichapa Coastal Mshindi wa Tatu Ngao ya Jamii

Simba Waichapa Coastal Mshindi wa Tatu Ngao ya Jamii


Bao pekee lililowekwa kimiani dakika ya 11 tu ya mchezo na kiungo mshambuliaji, Saleh Karabaka limeiwezesha Simba kumaliza nafasi ya tatu katika michuano ya Ngao ya Jamii, huku Kocha Fadlu Davids akipangua kikosi kilichopoteza mbele ya Yanga kwa kuwapumzisha nyota wanne na timu kutembeza boli la kisawasawa mbele ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union.


Simba iliyopoteza mechi na taji la Ngao ya Jamii ilipovaana na Yanga katikati ya wiki iliyopita, jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ilitembeza soka tamu lililowapa burudani mashabiki wa timu hiyo, wakati ikishinda bao 1-0 na kumaliza kama mshindi wa tatu wa michuano hiyo.


Karabaka alifunga bao hilo akimalizia mpira wa krosi ya Steven Mukwala iliyoguswa na Joshua Mutale na mfungaji huyo kukwamisha kwa shuti la karibu lililoshinda nguvu kipa Chuma Ramadhani aliyeanzishwa katika mchezo huo kuchukua nafasi ya Athuman Msekeni aliyepigwa mabao 5-2 na Azam visiwani Unguja.


DAKIKA 10 NGUMU


Katika pambano hilo, dakika 10 za mwisho zilikuwa za presha kwa wachezaji wa timu hizo, huku buti likitembezwa kwa timu hizo kiasi cha kuifanya Simba kumaliza ikiwa pungufu baada ya kiungo Fabrice Ngoma kuonyesha kadi ya pili ya njano iliyosindikizwa na nyekundu kutoka kwa mwamuzi Ramadhan Kayoko.


Ngoma atakosa mechi moja ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tabora United, kutokana na kadi hiyo baada ya kumchezea rafu mshambuliaji wa Coastal, Mbaraka Yusuph wakati anaenda kumsalimia kipa Moussa Camara, huko njano zikitoka kwa wachezaji wengine.


Licha ya Simba kucheza pungufu dakika 10 za mwisho ukichanganya na nne za nyongeza, ililinda bao hilo na kutangazwa mshindi wa tatu wa michuano hiyo.


Simba iliingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0, kutoka kwa wapinzani wao Yanga katika mchezo wa nusu fainali iliyopigwa Agosti 8.


MCHEZO ULIVYOKUWA


Simba ilianza mchezo kwa kasi kubwa ya kushambulia huku Coastal ikicheza kwa mikakati ya kujilinda ili isiruhusu mabao mengi kama ilivyowatokea katika mchezo wa nusu fainali ilipochapwa mabao 5-2 dhidi ya Azam FC, Uwanja wa New Amaan Complex Visiwani Zanzibar Agosti 8.


Licha ya Simba kushambulia kwa kasi na kupata bao la utangulizi dakika ya 10, kupitia kwa Saleh Karabaka ila nyota wa kikosi hicho walikosa utulivu wa kumalizia pasi za mwisho za kufunga.


Miongoni mwa nyota hao ni mshambuliaji mpya, Steven Mukwala aliyepata nafasi ya wazi dakika ya 19 na kushindwa kufunga, huku akikosa utulivu ambao ungeiwezesha timu hiyo kuongoza kwa idadi kubwa ya mabao katika kipindi kwanza.


Ukosefu wa utulivu kwa Simba ulimfanya kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids kuonekana wazi kumkera, kwani kuna wakati alikuwa anaonyesha mshangao kulingana na nafasi ambazo walikuwa wanakosa.


Kwa upande wa Coastal Union inayonolewa na Kocha Mkenya, David Ouma ilianza taratibu na hadi iliporuhusu bao la kwanza ndipo ilipoanza kushambulia, huku ikitengeneza nafasi mbili za wazi ambazo hata hivyo, hawakuweza kuzitumia vizuri wakiongozwa na mshambuliaji wa timu hiyo, John Makwatta.


FADLU APANGUA WANNE


Katika mchezo huo, kocha wa Simba, Fadlu alipangua kikosi katika nafasi nne kulinganisha na kile kilichoanza dhidi ya Yanga na kulala 1-0.


Kocha huyo Msauzi, aliyagusa maeneo mawili tu ya ulinzi na kiungo kwa kuwaweka nje, Shomary Kapombe, Chamou Karaboue, Mzamiru Yassin na Edwin Balua, akitoa nafasi kwa Kelvin Kijili, Abdulrazak Hamza na Augustine Okajepha na Saleh Karabaka aliowaanzisha.


Licha ya kuwa na uwezo wa kucheza kama beki wa pembeni, Hamza aliyetokea Supersport United ya Afrika kusini atatumika kama beki wa kati akicheza sambamba na Che Malone.


Kijili ambaye alingia kipindi cha pili katika dabi dhidi ya Yanga, ataendelea kutumika upande wa beki ya kulia huku kushoto akisalia nahodha wa kikosi hicho, Mohammed Hussein 'Tshabalala'.


Viungo wa kati ni Okajepha na Debora Fernandes ambao walicheza pamoja kipindi cha pili katika dabi, mawinga ni Karabaka na Joshua Mutale huku Jean Charles Ahoua na Steven Mukwala wakiongoza mshambulizi ya wekundu hao wa Msimbazi.


COASTAL WATANO


Kwa upande wa Kocha wa Coastal Union, David Ouma alifanya mabadiliko ya wachezaji watano tofauti na wale walianza siku walipopokea kipigo cha mabao 5-2 kutoka kwa Azam FC akiwapiga benchi kipa Athuman Msekeni na kumwanzisha Ramadhan Chuma pamoja na kuwaacha Felly Mulumba, Gerson Gwalala, Gift Abubakar na Abdalla Hassan na kuwaanzisha, Ramadhani Idd, Lukas Kikoti, Abdallah Denis na Denis Modzaka.


Mabadiliko hayo yalifanya timu kucheza kwa utulivu mbele ya Simba kulinganisha na ilivyocheza kwenye Uwanja wa Amaan Complex katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Azam, japo iliruhusu bao moja tu lililofungwa mapema na Saleh Karabaka na kuipa Simba nafasi ya tatu ya michuano hiyo ya Ngao ya Jamii.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad