Simba Wasipoangalia Vizuri Issue ya Aishi MANULA Inakwenda Kuwa Laana Kwao

 

Simba Wasipoangalia Vizuri Issue ya Aishi MANULA Inakwenda Kuwa Laana Kwao

Simba Wasipoangalia Vizuri Issue ya Aishi MANULA Inakwenda Kuwa Laana Kwao

Wakati ule wa usajili wa kutotumia mikataba, ilikuwa rahisi kwa klabu kutomwambia lolote mchezaji hadi siku ya mwisho ya usajili anapojikuta hayumo kwenye orodha ya klabu aliyokuwa anaichezea na kwa jumla hayumo kwenye usajili wa klabu yoyote hadi msimu mwingine.


Wakati huo hakukuwa na dirisha la katikati ya msimu. Usajili ulikuwa mwanzoni mwa msimu pekee. Hivyo mchezaji anayeachwa dakika za mwisho hukosa timu ya kuichezea hadi msimu mwingine unapofika. Wachezaji wengi waliteswa na ukatili huu wa viongozi, ambao wakati mwingine ulilenga kumkomoa mchezaji au kutokuwa na maamuzi thabiti yanayotokana na mikakati mizuri ya kuunda timu.


Lakini adha hii haikuwagusa wale wachezaji nyota kwa kuwa viongozi waliwawekea mikakati maalumu na hivyo mwishoni mwa msimu hawasumbuki. Wachezaji hao nyota nao walikuwa na mitego yao ya kuwakosesha kucheza msimu mzima.

Baada ya kusajili timu moja, nyota hao walibembelezwa hadi kukubali kusajili timu nyingine na matokeo yake yakawa ni kusajili timu mbili, kitu ambacho kikanuni hakikuruhusiwa na adhabu ikawa ni kufungiwa kucheza msimu mzima.

Hayo ni ya kale yalipita na ustaarabu wake kwa kuwa masuala ya mikataba yaliondoa tabia za viongozi kuwatelekeza wachezaji kwa sababu yoyote ile na iwapo hali hiyo itatokea, basi mchezaji ana haki ya kwenda kwenye vyombo vya haki kudai fidia au masuala mengine.

Ustaarabu wa kufuata na kuheshimu kanuni sasa umekuwa mkubwa na klabu zinazopuuza zinakumbana na adhabu kali za vyombo vya haki vya ndani au kimataifa kama vya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) au Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (CAS).

Utamaduni wa kizamani wa kutelekeza wachezaji ndio unaoonekana kumkabili kipa wa Simba na timu ya taifa ya Tanzania, Aishi Manula.

Katika utambulisho wa wachezaji kwa ajili ya msimu wa mwaka 2024/25, jina la gwiji huyo halikuwemo. Wako wengine ambao hawakutambulishwa kama Willy Onana na Israel Mwenda, lakini hawana uzito huo wa Aishi Manula.

Ingawa baadaye menejimenti yake iliwakumbusha wahusika na kuamua kumtaja, lakini tayari ilishakuwa fedheha kwa mchezaji ambaye ameitumikia Simba kwa miaka minane na kusaidia kuiwezesha kufikia mafanikio ambayo viongozi na mashabiki wanajivunia hii leo, ikiwemo kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mara nne na kutwaa ubingwa kwa miaka minne mfululizo.

Msemaji wa Simba Ahmed Ali alisema baada ya mechi ya Simba na APR Jumamosi kuwa Manula bado ni mchezaji wa Simba kwa mwaka mmoja zaidi na mwenye mamlaka ya mwisho juu ya hali yake ya baadaye kwenye klabu hiyo ni viongozi.

Ahmed pia alisema suala lake litapatiwa ufumbuzi kwa kuwa muda wa bado haujaisha, kauli inayoonyesha kuwa huenda klabu hiyo yenye m akao yake makuu Mtaa wa Msimbazi haina mpango wa kuendelea naye baada ya kutambulisha makipa watano Jumamosi.

Haitakuwa rahisi Simba kuwa na makipa watano msimu mmoja, huku watatu wakiwa wa viwango vya juu.

Ni tukio lililotokea wiki chache baada ya mchezaji mwingine aliyechangia mafanikio ambayo Simba inajivunia leo, John Bocco kuachana na klabu hiyo kwa njia ambayo inaonekana nahodha huyo wa zamani wa Simba hakuridhika na maamuzi ya viongozi ya kumpeleka kuwa kocha wa vijana wakati bado anaona anaweza kucheza soka la ushindani.

Kitendo cha kumsahau Manula katika utambulisho wa wachezaji, ni fedheha kwa kipa huyo wa kimataifa wa Tanzania na kulizungumzia suala lake bila ya kusahihisha kosa la kumsahau ni kutojali mchango wa lejendi huyo mwenye heshima yake katika soka la Tanzania.

Hata kama ataendelea kubaki, bado atakuwa na kinyongo akikumbuka tukio hilo na hali itakayofuata baada ya Simba kuunda kikosi kipya.

Si dhambi wala kosa la jinai kwa Simba kumuacha Aishi Manula au mchezaji mwingine yeyote aliyefikia daraja la gwiji au lejendi wa timu, bali njia inayoonekana kutaka kutumika kumuacha au vitimbi vilivyokwishatokea hadi sasa.

Msemaji wa Simba hakutaka kuzungumzia sababu za nyota huyo wa zamani wa Azam FC kuachwa safari ya maandalizi ya msimu Misri na sababu za kutokuwepo kambini kujiandaa na mechi ya Simba Day.

Ni Dhahiri kungekuwa na sababu zisizo na makandokando, msemaji angeshajua sababu hizo na isingekuwa shida kwake kuwaambia waandishi wa habari waliohoji sababu za kutokuwepo kwa kipa huyo aliyejijengea heshima ya kuwa ‘Tanzania One’.

Vitimbi kama hivyo vinaingia akilini mwake na kuacha vidonda ambavyo ni vigumu kupona.

Manula ana menejimenti yake inayosimamia mambo yake yote ya mikataba na maisha yake. Mchezaji kama huyu aliyekaa muda mrefu kwenye klabu moja na kuwa sehemu ya mafanikio hufanyiwa mazungumzo mapema kuhusu hali yake ya baadaye.

Maana yake, tangu msimu uliopita, Simba walitakiwa waanze mazungumzo na menejimenti yake kuhusu kutohitajika kwake katika mipango ya baadaye na kama kuna uwezekano apelekwe kwa mkopo sehemu ambayo anaona itamfaa kwa kipindi ambacho anakaribia kustaafu.

Mazungumzo hayo yakifanikiwa, maana yake atakapokuwa anarejea Simba, atarudi kwa roho nyeupe akijua ni sehemu ya familia ya klabu hiyo kubwa. Ndiyo maana, hata akirejea kucheza dhidi ya Simba akiwa na klabu nyingine, mashabiki huwapokea wachezaji kama hawa kwa heshima ya kusimama kuonyesha kuthamini mchango wake. Na kama ni mshambuliaji, huwa hashangilii bao anapoifunga timu ambayo amekuwa sehemu ya familia baada ya kuondoka kwa maelewano.

Manula anastahili heshima hii kama gwiji wa soka Tanzania na lejendi wa klabu kubwa kama Simba.

Ni muhimu Simba ikarekebisha kosa lililofanyika Jumamosi kwa kukaa naye na baadaye kutoa taarifa kwa umma itakayowatuliza mashabiki wamuone kipenzi chao kama mtu anayeondoka kiungwana au aliyekubali kusamehe kosa, kuepuka laana ya mtu aliyeipa mafanikio klabu lakini akaondolewa au kubakizwa klabuni kwa vitendo vinavyoonyesha kuna mauzauza.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad