Hakuna asiyejua kama Simba kwa sasa ni mpya. Timu hiyo iliyomaliza nafasi ya tatu msimu uliopita imeundwa upya. Ina benchi jipya kabisa la ufundi chini ya Fadlu Davids.
Imesajili wachezaji wapya 13. Ni zaidi ya kikosi kizima kuonyesha kwamba Simba kwa sasa ndo kwanza inaanza kujitafuta.
Kumbuka ni wiki kama mbili tu, imetoka kambini huko Ismailia, Misri ilikoenda kujifua kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano wa mwaka 2024-25.
Tangu timu hiyo ilipoenda kambini hadi iliporudi nchini, imecheza mechi sita tu zikiwa ni nne za kirafiki na mbili za kimashindano, ikiendelea kutafuta muunganiko.
Imechezesha mechi tatu za kirafiki za kujipima nguvu ikiwa Ismailia, Misri na kocha Fadlu alikaririwa akiwasifia wachezaji kwamba wameanza kumpa mwanga na pia kujisifia kwa kutopoteza mechi yoyote kati ya ilizocheza.
Ilianza kwa kuifunga Canal SC kwa mabao 3-0, kisha kushinda 2-1 dhidi ya Telecom Egypt na Al Adalah ya Saudia kwa idadi kama hiyo ya 2-1, kisha timu iliporejea nchini, imecheza mechi moja ya kirafiki katika Tamasha la Simba Day dhidi ya APR na kushinda mabao 2-0. Ulikuwa mwanzo mzuri, yaani mechi tatu mabao saba na kufungwa mawili, sio uwiano mbaya kwa timu inayojitafuta, hata kama haikucheza dhidi ya timu ngumu.
Ndipo sasa ikacheza mechi mbili za kimashindano ya Ngao ya Jamii 2024, ikianza dhidi ya Yanga na kulala 1-0 kabla ya kupata ushindi wa 1-0 mbele ya Coastal Union na kumaliza nafasi ya tatu katika michuano hiyo ya kufungulia msimu, huku Yanga ikibebea Ngao na Azam ikimaliza ya pili. Wastani pia sio mbaya kwani ni 1-1 katika mechi mbili zenye ushindani mkubwa.
STRAIKA MPYA
Mara baada ya mechi dhidi ya Yanga zilianza kuenea tetesi kwamba, kocha Fadlu anataka aongezewe mshambuliaji mpya. Mshambuliaji atakayekuwa akiifungia timu hiyo mabao na kuipa uhakika wa kushinda mechi.
Tayari inaelezwa Simba iko katika hatua za mwisho ya kusajili straika wa kukidhi kiu ya Fadlu, baada ya kutoridhishwa na washambuliaji waliopo kwa sasa kikosini.
Simba ina Mashaka Valentino iliyemsajili kutoka Geita Gold, ina Steven Mukwala kutoka Asante Kotoko ya Ghana, pia ni wachezaji waliokuwapo msimu uliopita kama Freddy Michael na Kibu Denis, mbali viungo washambuliaji na mawinga wenye uwezo wa kutupia mipira nyavuni.
Ina Saleh Kabaraka, Ladack Chasambi, Edwin Balua waliokuwapo tangu msimu uliopita, huku ikiwa na sura mpya za Omary Omary, Jean Charles Ahoua na Joshua Mutale. Debora Mavambo na Augustine Okejepha licha ya kuwa viungo wa ukabaji lakini pia ni wazuri kwa kufunga mabao.
Lakini kocha kaona bado anahitaji mshambuliaji wa kumaliza kazi ya kucheka na nyavu na viongozi wametii agizo na sasa wapo sokoni. Lipo jina la Lionel Ateba, Mcameroon anayetokea USM Alger ya Algeria anayesemekana kupewa mkataba wa miaka miwili huku kipa Ayub Lakred ambaye ni majeruhi akihusishwa na mpango wa kuondolewa kwenye usajili ili kumpisha straika huyo.
TATIZO WALA SIO HILO
Inawezekana ni kweli kocha Fadlu anaona wachezaji hawampi kile anachokihitaji kwa sasa, lakini ukweli ni kwamba hajaliangalia tatizo la msingi la timu hiyo kwa hatua hii ya mapema.
Simba hii mpya ambayo haina hata miezi miwili haina tatizo la straika. Ina tatizo la kutengeneza nafasi zitakazowarahisishia kazi washambuliaji kufunga mabao ya kutosha.
Fadlu na wasaidizi wake ni lazima wapitie upya mechi zote ambazo timu hizo imecheza kuanzia kule kambini Ismailia, Misri hadi ya juzi ya kusaka mshindi wa tatu dhidi ya Coastal Unioni iliyotoka kufumuliwa mabao 5-2 na Azam katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii.
Kwa wanaokumbuka Simba ilicheza mechi tatu za kirafiki Misri, ikianza na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Canal SC, huku ikipata mabao kupitia kwa Ahoua aliyefunga mawili na jingine la Okejepha.
Ikacheza mechi nyingine mbili dhidi ya Telecom Egypt na Al Adalah ya Saudi Arabia na kushindi kwa mabao 2-1 kila moja, wafungaji wakiwa ni Valentino Mashaka na Ladack Chasambi walipowaua Telecom na Steve Mukwala na Joshua Mutale wakawazamisha Wasaudia.
Kwa mechi zile ni ngumu kutoa tathmini kwa kikosi kilivyocheza kwani mechi ilikuwa ni ya ndani, lakini timu iliporejea na kucheza katika Simba Day na kushinda mabao 2-0 yaliyofungwa na Debora Mavambo na Edwin Balua, kila mtu aliona.
Simba haikutengeneza nafasi nyingi tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita ikiwa na wachezaji kama Saido Ntibazonkiza, Clatous Chama, Willy Onana, Babacar Sarr, Sadio Kanoute, Luis Miquissone na waliobaki kikosi cha sasa kama Kibu, Chasambi na Balua.
Bao la kwanza la Simba dhidi ya APR lililofungwa na Debora Fernandes, halikuwa la kutengeneza nafasi, kiungo huyo alitumia akili binafsi kwa kupiga shuti la kushtukiza kutokea mbali nje ya boksi mpira ukaenda wavuni na bao la pili lililofungwa na Balua, halikuwa la kutengeneza nafasi pia bali lilitokana na mpira wa kutengwa wa frii-kiki ya nje ya boksi iliyouvuka ukuta na kwenda moja kwa moja wavuni.
Dhidi ya Yanga, ilipolala kwa bao 1-0 timu haikutengeneza nafasi za kutosha, na ilipoiua Coastal Simba ilitengeneza nafasi moja ya maana iliyozaa bao lililofungwa Saleh Karabaka.
Kama timu haitengenezi nafasi, viungo hawawalishi washambuliaji, mabeki hawapigi krosi zinazowafikia kina Mukwala, ni lazima waonekane hawafai. Ni lazima Freddy na Mashaka waonekane uwanjani kama wakulima wanaokagua mashamba kwa kuzurura tu bila kuifungia timu mabao.
MUDA MFUPI MNO
Uamuzi wa Fadlu kutaka aletewe straika mpya kabla ya alionao kuwalisha mbinu na kuwakomalia kina Ahoua, Chasambi, Balua, Mutale na viungo washambuliaji wengine sambamba na mabeki wa pembeni kuwapa pasi na krosi zenye macho washambuliaji ni lawama ndani ya muda mfupi.
Wachezaji na hata kocha wana muda mfupi tangu waanze kuwa pamoja, hivyo kuwabebesha msala kina Mukwala ni kutaka kuwaonea tu, kwani hakuna pasi za kutosha za maana walizopewa eneo la lango la wapinzani kisha wakapoteza ili wapate kulaumiwa. Soka sio kama kukoroga chumvi katika mbona, ni mipango endelevu.
Hofu ni kwamba hata mshambuliaji mpya Msimbazi, iwe Ateba au yeyote atakayetua kabla dirisha la usajili halijafungwa leo usiku, kama hatalishwa mipira ataishia naye kulaumiwa tu kama Mukwala na wenzake.
Wanaomsaidia Fadlu ni lazima wamwambie ukweli kwamba Simba haitengenezi nafasi za mabao, kiasi cha kuona washambuliaji waliopo hawana uwezo wa kuibeba timu katika mashindano yaliyopo.
Timu ina muda mfupi tangu ijumuike pamoja na kufanya mazoezi kabla ya kucheza mechi hizo sita zilizopita ambazo huwezi kumhukumu mchezaji kama Mukwala aliyetoka Ghana akiwa na mabao ya kutosha. Ni ngumu kumsimanga Mashaka aliyetoka Geita akiwa kinara wa mabao, labda kama Fadlu amejishtukia kuwa Simba ni kubwa kuliko uwezo alionao na alivyoifikiria awali wakati akipewa kibarua angeweza kueleweka, kwani rekodi zinaonyesha kote alikofundisha alikuwa msaidizi tu na sio kocha mkuu.
Joto la kuwa kocha mkuu sasa ameanza kulihisi kwa klabu kubwa kama Simba ambayo mashabiki wake hawana uvumilivu, mambo yanaweza kumpalia mapema kuliko matarajio ya wengi. Angetuliza kichwa na kukomaliza kuwapa mbinu mawinga, viungo washambuliaji hasa Ahoua na mabeki wa pembeni kuwatengenezea nafasi nyingi washambuliaji ambao watajipanga katika eneo sahihi ili mambo yawe mepesi badala ya kuamini hawapati mabao kwa sababu ya kina Mukwala.
Ni lazima kocha Fadlu na wanasimba kwa ujumla kutoa muda zaidi ya wachezaji kuzoeana kwani ni wengi wao ni wapya na vijana wenye uwezo wa kushika maelekeo kwa ufanisi kadri muda utakapokuwa ukisonga mbele, pia wasijipe na ubora iliyonayo nayo Yanga, kwani watafeli mapema.
Yanga kwa misimu mitatu imezidi kuimarika na ina wachezaji waliozoeana kwa muda mrefu na wenye ubora tofauti na Simba mpya inayojengwa kwa sasa, ndio maana ni ngumu kumlinganisha Ahoua na maudambwidambwi aliyoondoka nayo Chama au wachezaji wengine waliopo Yanga. Simba ni timu nzuri inayojijenga kwa sasa, pia haina tatizo la mshambuliaji ila utengenezaji nafasi zitakazoweza kumalizwa na kina Mukwala katika nafasi sahihi. Hivyo tu, hayo mengine ni uzushi!