Treni ya abiria iliyokuwa ikisafiri kutoka Mkoani Kigoma kuelekea Dar es Salaam imepata ajali baada ya mabehewa sita (6) ya treni kuacha njia na kupelekea majeruhi 70, wanawake 26 na wanaume 44.
Taarifa iliyotolewa na Shirika la Reli Tanzania - TRC imeeleza kuwa Treni hiyo ilipata ajali kati ya Stesheni ya Kazuramimba na Uvinza mkoani Kigoma majira ya Saa 7.30 usiku wa kuamkia Agosti 28, 2024 na ilikuwa na jumla ya abiria 571 wakisafiri kutoka Kigoma kuelekea mikoa ya Tabora, Dodoma, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam na hakuna taarifa ya vifo vilivyotokana na ajali hiyo.
"TRC kwa kushirikiana na Kitengo cha Afya cha Mkoa wa Kigoma walifanikiwa kuwapeleka majeruhi katika hospitali ya Wilaya ya Uvinza kwaajili ya matibabu. Hali za afya za abiria zinaendelea kuimarika, majeruhi 57 tayari wameruhusiwa, nane (8) wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Wilaya ya Uvinza na watano (5) wamehamishiwa Hospitali ya Maweni kwaajili ya matibabu." - imeeleza taarifa ya @tzrailways