SIKU mbili baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumwondoa Ummy Mwalimu katika Baraza la Mawaziri, Mbunge huyo wa Tanga Mjini 'amefunguka', akimshukuru Mkuu wa Nchi kwa kumwamini na kumpa heshima ya kutoa huduma serikalini.
Mara tu baada ya kukabidhi ofisi kwa Waziri mpya wa Afya, Jenister Mhagama, Ummy aliandika katika ukurasa wake wa Instagram maneno ya kumshukuru Rais kwa namna alivyomwamini.
"Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka zake na kwa kila hatua tupitazo kwa kuwa zimezungukwa na neema zake ikiwamo kupata kibali cha kuitumikia nchi yangu katika nafasi ya Naibu Waziri (2010 - 2015) na Waziri (2015 hadi 2024). Si kwa uwezo au ujanja wangu, bali ni kwa ukuu wa Mungu.
"Pili, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa ninamshukuru Mheshimiwa Rais Samia kuniamini na kunipa heshima ya kuhudumu katika serikali yake katika nafasi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Machi 2021 hadi Januari 2022.
"Na Waziri wa Afya (Januari 2022 hadi Agosti 14, 2024). Asante sana Mheshimiwa Rais kwa imani na heshima kubwa uliyonipatia. Nitaenzi na kuitunza heshima hii daima," aliandika Ummy ambaye amehudumu Baraza la Mawiziri kwa miaka 14.
Aliendelea kueleza kuwa kwamba, kwa muda aliohudumu katika Wizara ya Afya, ameona ari, juhudi na kiu ya Rais Samia ya kuboreshea watanzania huduma za afya na wametoa mchango wao katika hilo.
"Yapo mengi tumeyasukuma na ambayo yanaendelea kusukumwa. Pongezi za dhati kwa dada yangu, Mheshimiwa Jenister Mhagama kwa kupokea kijiti.
"Sina shaka na uwezo, uzoefu na kujituma kwake katika kufikia malengo tuliyojiwekea pamoja na maono ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha upatikanaji huduma bora za afya kwa watanzania. Namtakia heri katika utekelezaji majukumu yake mapya," alisema.
Ummy ambaye amehudumu kwa muda mrefu katika wizara hiyo pia ameshukuru viongozi na watumishi wa wizara hiyo, wadau wa maendeleo na asasi za kiraia kwa ushirikiano mzuri waliompatia ambao alisema umewezesha nchi kupata matokeo chanya katika maeneo mbalimbali ya upatikanaji huduma za afya kwa wananchi.
"Shukurani za kipekee ni kwa wapigakura wangu wa Jimbo la Tanga Mjini kwa ushirikiano mzuri wanaonipatia na kwa uvumilivu wao mkubwa wakati wa utekelezaji majukumu yangu ya kitaifa.
"Asanteni sana wanaKimji. Nitaendelea kuwaenzi na kuwatumikia kwa ufanisi na sasa kwa karibu zaidi katika kuijenga Tanga yetu. Kazi kubwa iliyo mbele yetu sasa ni kutafuta ushindi wa kishindo wa CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025," alisema Ummy.
Baadhi ya wananchi walioandika katika ukurasa wake akiwamo anayejiita Malisa_gj, alimpa hongera pamoja na changamoto mbalimbali zilizoko katika sekta ya afya, akimweleza kwamba alijitahidi kutimiza yale yaliyokuwa ndani ya uwezo wake.
Wakati Susan_mlekia ameandika, "Hongera Odo (mama mdogo), wewe ni kiongozi mahiri na hakika ulijitahidi sana katika sekta ya afya nchini. Asante kwa utumishi mzuri, hakika wewe ni mfano wa kuigwa."