Moja kati ya kazi anayoipenda mno Haji Manara ni usemaji kwenye mpira wetu. Ndiyo maana kaifanya kwa kiwango cha juu kwenye klabu zetu mbili hapa nchini, Simba na Yanga.
Unamuona Haji Manara akijiunga na ile klabu? Bado natamani kumuona kwenye mpira, lakini sijui namuona wapi. Hakuna kitu kizuri kama kufanya unachopenda. Utakifanya vizuri. Hakuna kuchoka. Hakuna majuto.
Wachezaji wanaweza kutoka Simba kwenda Yanga, lakini haijawahi kutokea kwa viongozi lakini kwa Manara imewezekana. Alitoka Simba kama mfalme wa wasemaji na kwenda Yanga kwenye ufalme mwingine.
Kila mtu na kazi yake. Kila mtu na kipaji chake. Karibu vijana wengi wa kizazi hiki wanaosemea klabu wanapita njia zilezile za Haji. Kuna kiwango kwenye eneo hili huwezi kuvuka bila kupita njia zake. Amekuwa ni fundi wa kipaza sauti. Haji anajua sana mpira. Ana mbwembwe sana. Anajua vizuri siasa za soka letu. Ukiwa timu pinzani hakuna mtu anakera kama yeye.
Twende mbele, turudi nyuma. Haji ameongeza sana thamani ya mpira wetu. Kuna watu walikuwa siyo wapenzi kabisa wa soka, lakini mdomo wa Haji wanaupenda. Wanafurahia propaganda zake. Haji amekuwa mtu mwenye kifua pia. Kila timu yake inapofungwa au kutolewa mitandao yote imekuwa ikimzodoa nchi nzima. Mashabiki wa soka wamemfanya kama babu yao. Ni utani mwanzo mwisho.
Kulikuwa na mkanganyiko mkubwa baada ya adhabu ya Haji kufungiwa kujihusisha na mpira kumalizika. Haji kabla ya kufungiwa alikuwa msemaji wa Klabu ya Yanga. Kabla ya kufungiwa Yanga walimwajiri Ali Kamwe. Rais wa Yanga, Hersi Said wiki iliyopita aliamua kutegua kitendawili hicho kwa kutangaza rasmi kuwa msemaji anayetambulika ni Kamwe na Haji ni mwanachama tu kama wanachama wengine.
Ilikuwa ni taarifa njema kwa waliokuwa wanaumizwa na vijembe vya Haji. Ilikuwa ni taarifa mbaya kwa wanaofurahia burudani na sanaa ambayo Haji amekuwa akiitumia. Haji ameongeza sana thamani ya idara ya habari kwenye klabu zetu. Tofauti kubwa ya Haji na wasemaji wengine anajua sana mpira na siasa zake.
Siasa za Simba na Yanga zinahitaji mtu kama yeye kuweza kuzisimulia. Haji ni mtoto wa mjini pia ambaye nakshi nakshi zake zinaongeza burudani. Haji ametumika kuwapa imani mashabiki na kuwaaminisha kuwa kwenye soka hakuna kisichowezekana.
Kuna watu wamekuwa wakienda uwanjani baada ya maneno yake. Hata wachezaji kuna namna wamenufaika sana na uwezo wa Haji. Amekuwa akitumia zaidi mitandao yake ya kijamii kuwapa promo wachezaji. Amekuwa akipambana sana mitandaoni na watu wanaoshambulia timu yake. Sidhani kama Haji amemaliza kwenye eneo hilo. Sidhani kama atakubali kuondoka mazima kwenye eneo la usemaji. Unamuona Haji Manara akijiunga na Singida Black Stars? Kwa mtoto wa mjini sioni hilo likitokea. Bado natamani kumuona kwenye mpira, lakini sijui namuona wapi. Unamuona Haji akirudi Simba? Sidhani. Kwa namna alivyoondoka na watu aliowaacha ni walewale. Sioni Kama hili jambo linawezekana kirahisi. Vipi kuhusiana na uwezo wa Ahmed Ally? Nadhani ameshajipata. Ahmed anapiga kazi kubwa kwelikweli. Azam FC? Nako shughuli ipo. Haji anapenda kupasuka sana mbele ya kipaza sauti kitu ambacho sidhani kama Azam FC wanataka. Zaka Zakazi na Hasheem Ibwe nao naona wanaupiga mwingi. Haji ni fundi sana eneo la propaganda na siasa za mpira. Pale Azam FC sio watu wa siasa. Sio watu wanaotaka vurugu za Simba na Yanga.
Unamuona Haji akienda Azam FC? Mimi napata shaka. Vipi tunaweza kwenda kumuona akitokea TFF? Hata hapo sidhani. Uhusiano wake na rais wa TFF, Wallace Karia siyo mzuri sana. Uhusiano wake na katibu wa TFF, Wilfred Kidao naona pia siyo mzuri sana. Simuoni akienda Karume. Simuoni kabisa. Idara ya habari pale TFF ni kama imepoa kidogo, lakini uhusiano mzuri na watu ni jambo la msingi.
Nadhani tunahitaji mtu kama Haji wa kuisemea TFF na timu zetu za Taifa. Tunahitaji mtu wa kidijitali wa kucheza na maneno, lakini simuoni Haji hapo. Sitaki kuamini kuwa Haji ndiyo basi tena. Namuona akirudi tena kwenye usemaji, lakini sijui ni klabu gani.
Umewahi kuiwaza Singida Black Stars (SBS)? Huwezi jua. SBS ni moja kati ya timu zilizofanya usajili mzuri na wanaonekana kuwa na bajeti ya kutosha. Sioni kama ni rahisi kwa mtoto wa mjini kwenda kuishi Singida, lakini maisha ni popote.
Bado nikiutazama mpira naona bado kuna nafasi ya Haji. Bado msemaji kama Haji ni muhimu sana kuongeza morali kwa mashabiki na baadhi ya wachezaji ambao hawamudu presha kubwa.
Mpira wetu bado nguvu yake kubwa ipo kwenye siasa zake. Unahitaji mtu anayezijua vyema siasa zile na mwenye ushawishi mkubwa. Sitaki kuamini kuwa zama ndiyo zimeisha. Siamini kama Haji ndiyo hatausemea tena mpira wetu. Bado namuona akirejea kwa kishindo na kuupambania mpira. Uliwahi kuamini kama Haji ataiacha Simba na kwenda Yanga? Usinipe jibu. Basi usimalize maneno, usijeshangaa siku moja ukamuona tena Haji Msimbazi. Mambo yanabadilika.
Maisha ni mabadiliko. Nilimsikia rais wa Yanga, Hersi Said akisema kuwa kamati ya utendaji itaangalia nafasi ambayo Haji inamfaa. Kwa maoni yangu, hakuna nafasi nyingi yoyote inayomfaa zaidi ya usemaji. Kama tayari Yanga wameshajipata kwa Ally Kamwe nadhani shughuli iishie hapo. Unamuona Haji Manara akijiunga na Singida Black Stars? Kwa mtoto wa mjini sioni hilo likitokea. Bado natamani kumuona kwenye mpira, lakini sijui namuona wapi.