Ingawa kuimarika kwa huduma za treni ya umeme nchini Tanzania ni furaha kwa abiria, kwa upande wa wamiliki wa mabasi ni maumivu, wakilalamika juu ya kudorora kwa biashara.
Malalamiko ya wasafirishaji hao yanakuja katika kipindi ambacho, safari za treni ya umeme zinazidi kuimarika na leo Alhamisi, Agosti 1, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi safari kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Hata hivyo, kinacholalamikiwa na wasafirishaji hao, kimeelezwa na Rais Samia akisema kwa namna yoyote lazima wasafirishaji kwa njia ya mabasi waathirike, lakini wanayo fursa ya kwenda katika maeneo ambayo treni hiyo haifiki.
Msingi wa malalamiko ya wasafirishaji hao ni kile wanachoeleza, wanakosa abiria na hivyo kuathirika kibiashara, jambo linalochochewa na uwepo wa treni ya umeme.
Malalamiko hayo yameibuka leo Alhamisi, Agosti 1, 2024 na Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo katika mahojiano yake na Mwananchi.
Mwananchi liliwatafuta Taboa kupata mtazamo wao juu ya kile alichokieleza Rais Samia kuwa anatambua uwepo wa treni ya umeme inakwenda kuwaathiri wenye mabasi. Rais Samia amesema hayo akiwa ndani ya treni mara tu baada ya safari kuanza kutoka Dar es Salaam.
Alipofika Morogoro mkuu huyo wa nchi alizungumza na wananchi mbalimbali waliokuwapo hapo na alitumia fursa hiyo kumwita Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdul-Aziz Abood na kumweleza atafute maeneo mengine sasa.
Abdul-Azizndiye mmiliki wa Kampuni ya mabasi ya Abdul Abood na wakati akieleza hayo huku wakishikana mikono alionekana kufurahia.
"Kuwepo kwa reli hii mdogo wangu Abood ataumia, na taarifa niliyonayo mdogo wangu Abood kashapunguza mabasi yake barabarani, lakini mdogo wangu Tanzania hii ni kubwa unaweza kupeleka mabasi yako maeneo mengine," amesema Samia.
"Hiyo ndio shida na raha ya maendeleo, kingine kitaathirika kingine kitakwenda," amesema.
Rais Samia amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye mradi huo ambapo Sh10 trilioni kimetumika kukamilisha ujenzi wa reli hiyo kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma.
Amesema lengo ni kufika hadi mkoani Kigoma na nchi jirani ya Burundi na DR Congo.
‘Abiria wanachagua treni’ Katika mahojiano na Mwananchi, Mwalongo amesema abiria kwa sasa wanachagua kupanda treni badala ya mabasi, hivyo wamiliki wa usafiri huo na wafanyakazi wao kwa ujumla wanaathirika.
Kuathirika huko kunatokana na kile alichoeleza, nauli iliyopangwa katika usafiri wa treni haijapishana na basi, ilhali huduma za vyombo hivyo vya usafiri ni tofauti.
Amesema abiria anapopanda basi anatumia saa saba kufika Dodoma, wakati akipanda treni ni saa tatu pekee na kwa sababu nauli zinafanana hakuna atakayechagua kuchelewa.
“Treni imekuja kutufukuza watu wa mabasi, kwa sababu nauli zilizopangwa ni karibu zinafanana na wao wanatumia njia moja, muda mfupi zaidi, kwa hiyo nauli ilipaswa kuwa tofauti treni ingekuwa kubwa,” amesema.
Kwa mujibu wa Mwalongo, athari ni kubwa na kulipaswa kuwepo mazungumzo kati ya Serikali na watoa huduma wa mabasi kuona namna ya kwenda.
“Athari ni kubwa na ukubwa wake ni pale ambapo treni inapoonekana imejaa hawasemi imejaa wanaongeza behewa lingine, huyo atakayekuja kupanda basi atumie saa saba nani.
“Hatukatai maendeleo na siku zote huwa na changamoto lakini Serikali ilipaswa kutuita na kutafuta maneno mazuri ya kutwambia kama haitutaki tena,” amesema. Kuhusu fursa ya kwenda katika maeneo mengine kutoa huduma hiyo, Mwalongo amesema Tanzania yote hakuna eneo lisilo na huduma ya mabasi, hivyo uwezekano wa kuongeza mabasi maeneo mengine ni mgumu.
Sambamba na hilo, amesema uanzishwaji wa safari mpya unagharimu mamilio ya fedha, jambo ambalo wasafirishaji wanaliogopa.
Kwa malori kicheko Lakini kwa upande wa malori, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki Wadogo wa Malori (Tamstoa), Chuki Shaaban amesema uwepo wa treni hiyo ni fursa kwao.
Fursa hiyo itatokana na kile alichoeleza, eneo linakofika lori treni haina uwezo wa kufika, hivyo wataendelea kufanya kazi wanayoendelea nayo na pengine ikaongezeka zaidi.
Kwa mujibu wa Shaaban, ujio wa treni hiyo utaongeza mizigo bandarini na hivyo malori yatakuwa na kazi nyingi za kupakia kupeleka kwa wamiliki.
“Treni itabeba mzigo hadi kwenye bandari na wakati mwingine itaishia bandari kavu, ili kuufikisha kwa mmiliki lori ndilo litakaloifanya kazi hiyo, kwa hiyo sioni athari zaidi ya fursa,” ameeleza.
Amelisisitiza hilo kwa ufafanuzi kuwa, Ulaya kuna treni nyingi zaidi zinazosafirisha mizigo, lakini bado malori ni mengi kwa ajili ya shughuli zake. “Sisi tunapongeza kwa ujio wa treni, tunaamini kazi zitaongezeka zaidi,” amesema.