ALIYEKUTWA AMEKUFA KWENYE RANGE ROVER MAGOMENI NI MUOSHA MAGARI


ALIYEKUTWA AMEKUFA KWENYE RANGE ROVER MAGOMENI NI MUOSHA MAGARI

Gari la aina ya Range Rover likiwa limeegeshwa eneo la Magomeni Mapipa ambalo ndani yake umekutwa mwili wa mwanaume ambaye bado hajatambulika.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, limemtambua Seif Hamad ambaye mwili wake ulikutwa ndani ya gari katika Mtaa wa Idrisa Magomeni Mapipa, jijini Dar es Salaam.

Mwili wa Hamad, maarufu ‘kikeri’ ulikutwa katika gari hilo, aina ya Range Rover HSE.

Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro ameliambia Mwananchi leo Jumatano Septemba 25,2025 kuhusu mwenendo wa tukio hilo, akisema kuwa mwili wa Kikeri ulifanikiwa kutolewa ndani ya gari hilo jioni ya jana Jumatano Septemba 24, 2024.

“Unajua watu wakiendea kuosha magari wanaacha funguo, sasa Kikeri ni muosha magari pale Magomeni, ile gari bado mpya, lakini tunachoamini baada ya kuliosha aliingia ndani akafunga mlango na kulala.”

“Kumbuka lile ni Range ambalo lina remoti kama hulijui huwezi kulifungua, kwanza ukilala ndani yake sio rahisi kujua hadi mwenye gari awepo, sasa mmiliki wa Range alikwenda safari ya siku mbili Zanzibar na aliliacha gari lake lioshwe,” amesema Kamanda Muliro.

Kamanda Muliro amesema ndiyo maana ilikuwa ngumu watu kubaini kwa haraka kama ndani ya gari hilo kuna mtu amelala hadi harufu ilipoanza kutoka nje.

“Bado polisi tunaendelea na uchunguzi wa kifo hiki, lakini mazingira yake yapo hivi, kwa sababu hata funguo ya gari alikutwa nayo ndani, ukimuachia mtu gari aoshe maana yake asogeze, sasa huyu (Kikeri) akaamua kulala na kufunga milango ambayo inawezekana ilimshinda kufungua.

“Huu ni uchunguzi wa awali bado tunaendelea kuchunguza pia lakini ukweli upo hivyo,” amesema Kamanda Muliro.


Eneo ambalo gari hilo bado halina namba ya usajili wa Tanzania ni maarufu kwa uuzaji wa magari ya aina mbalimbali.

Jana Jumanne, Mwananchi lilifika katika eneo hilo na kukuta askari Polisi wakifanya jitihada za kufungua milango ya gari kitendo kilichochukua zaidi ya nusu saa.

Kabla na baada ya kuifungua milango ya gari hilo askari Polisi na wataalamu wa afya waliokuwa eneo hilo, walilazimika kupuliza dawa ili kupunguza harufu iliyokuwa ikitoka katika gari hilo.


Baada ya kufanikiwa kufungua mlango, mwili wa Kikeri ulikuwa eneo la buti ukiwa kifua wazi huku simu yake janja ikiwa miguuni pake.

Mwandishi wa Mwananchi aliyekuwa eneo la tukio akishuhudia ufunguaji wa gari hilo, alieleza kuwa mwili wa marehemu ulionekana kama umelala kwa staili ya kujikunja huku ukiwa umevimba.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad