AZAM MEDIA HAIKUPASHWA KUSUSIA NDONDI

 

AZAM MEDIA HAIKUPASHWA KUSUSIA NDONDI

Mabondia, wapenzi wa ngumi na wanamichezo kwa sasa wamepigwa na butwaa baada ya Kampuni ya Azam Media kutangaza haitajihusisha tena na urushaji wa matangazo ya moja kwa moja ya mchezo huo.


Uamuzi huo umetokana na Azam kushindwa katika kesi ya madai ya haki miliki iliyofunguliwa na bondia wa zamani, Amosi Mwamakula, aliyedai mahakamani kampuni hiyo iliiba wazo lake la kuendesha mapambano ya ngumi za kulipwa na kurushwa moja kwa moja na televisheni.


Mwamakjula alidai asili ya programu ya Vitasa ni wazo lake aliloliwasilisha Azam na kukubaliana waanze kurusha mapambano hayo, huku bondia huyo akiwa ameshasajili mpango huo kwa ajili ya haki miliki.


Mara baada ya utekelezaji wa mpango huo kuanza, Mwamakula anadai alielezwa na wahusika wa Azam wazo hilo lililokuwa limewasilishwa kielektroniki, halionekani na baada ya muda Azam wakaibuka na mpango huo wa Vitasa, ambao bondia huyo anadai kila kitu kiliigwa kutoka katika wazo lake.


Ndipo aliposhtaki Chama cha Haki Miliki Tanzania (Cosota) ambako walimwambia ni mawazo kufanana, lakini hakuishia hapo kuitafuta haki yake hadi Azam ilipoamriwa imlipe Sh200 milioni.


Ingawa kuna habari Azam itakata rufaa, lakini imeshaweka wazi haina mpango wa kuendelea na ngumi za kulipwa.


Taarifa hiyo imewashtua wengi, hasa baada ya mchezo huo wa ngumi za kulipwa kurejea kwa kasi nchini baada ya Azam kuanza kurusha mapambano hayo moja kwa moja na hivyo kuondoa ukiritimba wa mchezo wa soka ambao kutwa kucha unazungumziwa, kibaya zaidi, habari hizo ni za Simba na Yanga sana.


Azam ilikuwa imerejesha enzi za kina Rashid Matumla na ndugu zake ambao kwa kiasi kikubwa, wakishirikiana na kampuni ya DJB Promoters, waliupandisha mchezo wa ngumi za kulipwa na kusababisha vijana wengi kuupenda na kuanzisha klabu nyingi mitaani.


Tulitarajia uamuzi wa mahakama uchukuliwe kama ajali kazini kwa kuwa ni vitu vya kawaida kwa vyombo vya habari kuingia kwenye majanga kama hayo ya kushtakiwa na kutakiwa kulipa mamilioni ya fedha kwa watu ambao ama wanadai kudhalilishwa au madai mengine.


Kwa kawaida majanga kama hayo yanapotokea, vyombo vya habari huimarisha uhariri ili kupunguza uwezekano wa watu kudhalilishwa au makosa mengine na zaidi kuendesha mafunzo ili waandishi wajifunze kutokana na makosa yaliyosababisha hasara hiyo.


Kama kulikuwa na makosa ya kizembe, basi waliosababisha huchukuliwa hatua stahiki ili iwe fundisho kwa wengine, pia kuwakumbusha wajibu wao kwa jamii.


Ungetarajia hilo litokee kwa Azam Media. Huku ikifikiria kukata rufaa, ilitakiwa ianze kujitathmini kwa ndani kujua kama kweli Mwamakula aliwasilisha wazo hilo na ilikuwaje kampuni ikaachana nalo ghafla na kuanzisha wazo kama hilo hilo bila ya kuchukua tahadhari za kisheria zinazohusu haki miliki.


Kwa kawaida maudhui kama hayo yakifanywa moja kwa moja na kampuni ya utangazaji, basi huhusisha gharama kubwa na ndiyo maana maudhui kama hayo huandaliwa na kampuni nyingine na uandaaji matukio na kuuza haki za matangazo kwa kampuni za utangazaji.


Yaani ni sawa na Shirikisho la Soka (TFF) kuwa na mashindano yake kama Ligi Kuu, Ligi ya Championship, First League, Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) na nyingine za vijana, halafu Azam inakuja kununua haki hizo za matangazo na kuepukana na hekaheka za kuandaa mashindano yake.


Ndivyo ilivyo duniani kote, kampuni ya utangazaji inanunua maudhui au kutoa muda wa hewani kwa taasisi au mtu aliye na wazo la kipindi chake na baadaye kujadiliana jinsi ya kugawana malipo kadri kipindi hicho kinavyovuta watazamaji.


Mbali na biashara, utangazaji pia ni huduma kwa jamii hivyo ile inayoonekana kama ni hiari au utashi wa kurusha maudhui fulani, huepukwa pale kampuni inapoamua kujihusisha na shughuli za kijamii. Wakati mwingine huonekana kama wajibu.


Azam haikupaswa kukimbilia kutangaza kuachana na ngumi za kulipwa kwa sababu bondia mmoja ameishtaki na kushinda kesi. Uamuzi huo ni kususa, kitu ambacho usingekitarajia kwa kampuni kubwa kama Azam Media ambayo inaongozwa kwa kufuata miongozo na kanuni za mashirika makubwa (corporate governance).


Ungetarajia uamuzi kama huo wa kuachana na mchezo huo unaozidi kukua, usubiri taratibu za vikao vya bodi, ambayo kwa kawaida hujadili shauri kwa mapana na marefu yake kabla ya kufikia uamuzi kama huo.


Hakuna shaka Azam imeshiriki kwa kiasi kikubwa kukuza michezo nchini, hasa soka, mpira wa kikapu na ngumi za kulipwa.


Hivyo sifa yake ya kushiriki kusisimua na kuiamsha baadhi ya michezo, isitiwe doa na mtu mmoja ambaye aliamua kutumia vyombo vya haki kudai kile anachokiona ni haki yake.


Kwenda mahakamani si kuichafua Azam bali kudai haki kihalali kabisa kwa kutumia vyombo vilivyowekwa kisheria huku kila upande ukipewa nafasi sawa ya kujenga hoja kujitetea.


Matumaini yetu ni Azam Media itaghairi uamuzi wake wa kuachana na ngumi za kulipwa na kutengeneza mazingira yatakayozuia hali kama hiyo kutokea baadaye. Kuamua kutotangaza ni kususia mabondia, kususia vyama vinavyoongoza mchezo huo, kususia wapenzi wa ngumi, kususia wapenzi wa michezo na Watanzania wapenda mema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad