Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa taarifa zikiambatana na picha pamoja na video asubuhi hii kuwa Nyumba wanazoishi Viongozi wake ambao ni Mwenyekiti Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu zimezingirwa na Askari Polisi tangu jana usiku ikiwa leo ndio siku iliyopangwa kufanyika maandamano ya amani ya maombolezo ya haki.
Taarifa iliyotolewa na Chama hicho kuhusu nyumbani kwa Mwenyekiti Freeman Mbowe imesomeka kama ifuatavyo ———> “Tangu jana usiku mpaka asubuhi ya leo Septemba 23, 2024 Jeshi la Polisi limefunga barabara zote zinazoelekea nyumbani kwa Mwenyekiti wa Chama Taifa Mhe. Freeman Mbowe, Watumiaji wote wa barabara hiyo wanasimamishwa na kukaguliwa, wakiulizwa kama wanakwenda kwenye maandamano #maombolezoyahaki”
Taarifa kuhusu nyumbani kwa Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu imeeleza yafuatayo ———> “Asubuhi hii Jeshi la Polisi limezingira nyumbani kwa Makamu Mwenyekiti Bara Mhe. Tundu Lissu, #MaombolezoyaHaki”
Taarifa nyingine imeuonesha ujumbe wa Katibu Mkuu John Mnyika akiwa ameuandika kwenye karatasi kwa mkono ukisomeka ———> “Naamini kwa nguvu ya Mungu mmeamka salama na ujasiri wa kufanya maombolezo ya haki kupitia maandamano ya amani, ni maombi yangu wote mfike kwa wakati saa 3 kamili Magomeni Mapipa na Ilala Boma Sokoni kuelekea Viwanja vya Mnazi Mmoja, nimepata taarifa wachache watakaovalishwa sare za CHADEMA waanzishe fujo kuhalalisha Polisi kufanya udhalimu, wadhibitini mapema kwa maadili na amani ya nguvu ya umma” #MillardAyoUPDATES