Chelsea ilituma ofa ya kumnasa straika Victor Osimhen saa za mwisho kabla ya dirisha la usajili kufungwa usiku wa kuamkia jana Jumamosi, lakini ilishindwa kufanikisha dili hilo baada ya Mnigeria huyo kuwachunia, imeelezwa.
Chelsea ilikuwa bize katika siku ya mwisho ya dirisha la usajili. Ilifanikiwa kumnasa kwa mkopo winga Jadon Sancho kutoka Manchester United, wakati ikimtoa pia kwa mkopo Raheem Sterling kwenda Arsenal, ambapo dili hilo lilitangazwa saa tatu baada ya dirisha kufungwa.
Lakini, kwenye dili la Osimhen, Chelsea imeshindwa kunasa saini ya fowadi huyo ambaye alikuwa akisakwa na timu hiyo kwa miezi kibao.
Kwa mujibu wa Sky Sports, Chelsea ilipeleka ofa dakika za mwisho kumsajili Osimhen, lakini hawakupata jibu lolote kutoka kwa straika huyo wa Super Eagles.
Kulikuwa na ripoti kwamba mabosi wa Chelsea walisafiri kwenda Naples, juzi Ijumaa kumshawishi Osimhen awe The Blues.
Kwenye mchakamchaka huo, Chelsea ilikuwa ikishindana na Al-Ahli ya Saudi Arabia, ambapo ilielezwa kwamba miamba hiyo ya Mashariki ya Kati ilishafikia makubaliano ya kuilipa Napoli, Pauni 67 milioni.
Osimhen alionekana kuwa tayari kuondoka Napoli, lakini mahitaji ya kutaka alipwe mshahara wa Pauni 500,000 kwa wiki, hakuna timu yoyote si Chelsea wala Al-Ahli iliyokuwa tayari kulipa kiasi hicho.
Chelsea ilikuwa na matumaini Osimhen angekubali kulipwa bonasi na marupurupu kuliko mshahara. Mashabiki wa Chelsea waliripotiwa kuchukizwa na madai ya kwamba Chelsea iliweka mezani ofa ya mshahara wa Pauni 130,000 kwa wiki ili kumchukua Osimhen. Inaelezwa, hilo ndilo lililomfanya straika huyo asiwasikilize kabisa mabosi wa Chelsea pamoja na jitihada zao za kumsajili kwenye dakika za mwisho.
Chelsea imegonga mwamba pia kwenye usajili wa straika Ivan Toney baada ya fowadi huyo wa Brentford kusajiliwa na Al-Ahli ya Saudi Arabia.