Ni nadra sana wachezaji kukubali uwezo wa wapinzani wanaocheza nafasi moja uwanjani, lakini ni tofauti kwa beki wa Azam FC, Nathaniel Chilambo anayemtaja staa wa Yanga, Attohoula Yao ni darasa kwake kutokana na uwezo mkubwa wa mchezaji huyo.
Chilambo amefunguka hayo kwenye mahojiano maalum na Mwanaspoti pamoja na mambo mbalimbali ikiwamo nafasi finyu ya kucheza katika kikosi cha Azam FC kwa kuwekwa benchi na Lusajo Mwaikenda.
YAO KAONGEZA KITU
Ikiwa ndiyo msimu wa pili kwa Yao Yanga, ameshinda mataji mawili ya ndani la Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho, akianza pia na Ngao ya Jamii msimu huu na ameonyesha kiwango bora na kuwa miongoni mwa nyota wanaotazamwa zaidi na Chilambo.
“Kuna mabeki wengi wazuri kuanzia wa ndani kama Mwaikenda anayefanya vizuri Azam FC na timu ya Taifa, Kibwana Shomari lakini kwa wageni kuna Yao ni beki anayefanya kazi nzuri na kuna kitu cha kujifunza kwani amekuja kuongeza thamani kwenye ligi yetu,” anasema na kuongeza;
“Navutiwa na aina ya uchezaji wake, pia kuna kitu cha tofauti amekionyesha. Tunacheza nafasi na nimekuwa nikimfuatilia na kujifunza mazuri kutoka kwake.”
KAPOMBE BADO TUNAMHITAJI
Wakati wadau wengi wa soka wakidai beki wa Simba, Shomari Kapombe umri umemtupa mkono kutokana na kucheza kwa muda mrefu, Chilambo anasema bado ana nguvu na uwezo wa kufanya vizuri.
“Msafara wa mamba kenge hakosi, hivyo ndivyo naweza kusema kutokana na maneno yanayosemwa juu ya Kapombe. Kwa upande wangu naona bado ana nguvu na ubora tatizo ni watu wamemchoka lakini kazi bado inamhitaji kutokana na ubora alionao,” anasema na kuongeza;
“Kuna siku mbaya kazini. Anapofanya vibaya ndiyo maneno mengi yanawatoka lakini akifanya vizuri wanakosa maneno. Mimi naamini katika upambanaji wake na ni miongoni mwa mabeki ninaowafuatilia.”
Chilambo anasema Kapombe ni mchezaji ambaye amekuwa na ubora licha ya kucheza muda mrefu na anafanya kazi yake bila kujali maneno ya watu licha ya kusemwa amekuwa akiwajibu uwanjani, ujasiri ambao anatamani kuwa nao hata yeye ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufikia malengo.”
KIUNGO HADI BEKI
Sio wachezaji wote nafasi wanazocheza walianza kucheza hapo, japo kuna wengine ni viraka wanacheza nafasi zaidi ya nne uwanjani. Kwa upande wa Chilambo alianza kucheza kiungo na winga sasa anacheza beki namba mbili.
“Nafasi ninayocheza nimebadilishwa na Charles Boniface Mkwasa. Mwanzo nilikuwa nacheza winga zote na kiungo mshambuliaji na mkabaji lakini kwa kuwa kocha ndiye anatambua vipaji, aliniamini na kunibadili nafasi,” anasema na kuongeza;
“Mwanzo nilikuwa nachukia kucheza hii nafasi lakini sasa ndiyo nafasi ninayocheza na naifurahia.”
Chilambo anasema licha ya kuzoea nafasi hiyo lakini ikitokea akapangwa nyingine atacheza na kufanya vizuri kwa sababu soka ndiyo kazi yake na hawezi kuchagua nafasi ya kucheza japo amejiunga na Azam FC baada ya kuonyesha uwezo katika nafasi ya beki na mazoezini amekuwa akijifua zaidi eneo hilo.
YANGA IMENITAMBULISHA
Ni nadra kwa mchezaji kupandishwa kutoka timu ya vijana na akapangwa kikosi cha kwanza kuikabili timu kubwa kama Yanga, lakini Chilambo anakiri chini ya Mkwasa haikuwa ngumu kwani aliaminiwa na kupangwa mechi dhidi ya Yanga.
“Mkwasa aliniamini na kunipandisha timu ya wakubwa. Alinipanga kucheza nafasi hiyo dhidi ya Yanga, mechi ya ligi kabla ya Ruvu Shooting kushuka daraja,” anasema na kuongeza;
“Haikuwa rahisi lakini ndiyo ilikuwa hivyo, nakumbuka mchezo ulipigwa Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salam tulifungwa 3-1 kama sijakosea, ilikuwa ngumu kwangu na nilikuwa nachukia hiyo nafasi.”
Anasema mechi hiyo ndiyo ilikuwa ya kwanza kucheza nafasi hiyo na licha ya kuichukia sasa ndiyo imemtambulisha na imempa ulaji Azam FC anayoitumikia sasa.
“Kwa sasa naifurahia hii nafasi na endapo ikitokea nikipata nafasi ya kupangwa eneo tofauti na nilalocheza sasa nacheza. Mimi ni mchezaji, kocha akiona nafiti nafasi yoyote nacheza kwa sababu hata beki sikutegemea kama nitaweza,” anasema.
BOCCO, SAMATTA MUDA BADO
Wakongwe wa soka nchini na manahodha kwenye kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ John Bocco na Mbwana Samatta kwa nyakati tofauti wametangaza kustaafu kuichezea timu hiyo kitendo ambacho hakijaungwa mkono na Chilambo anayekiri bado mchango wao unahitajika.
“Samatta na Bocco ukiachana na timu zao wamefanya mambo makubwa sana Stars na bado tunaamini wana nguvu za kuendelea kulitumikia taifa japo wamefanya uamuzi ambao pia unatakiwa kuheshimika,” anasema na kuongeza;
“Stars inahitaji wachezaji wazoefu licha ya damu changa pia kuwa na nafasi lakini uwepo wa kına Bocco na Samatta utasaidia ushirikiano zaidi kimawazo na hata vitendo na vijana ili kutujenga na sisi tufikie mafanikio kama wao.”
Anasema kwa mapenzi yao wameomba kustaafu lakini yeye kama mchezaji kijana anaamini wakongwe hao bado wanahitajika kuendelea kuwapa muongozo kwa kuwajenga ili na wao wawecheze muda mrefu na kwa mafanikio.
MKWASA BADO ANAMUAMINI
Sio rahisi kwa makocha wote kukumbuka vipaji walivyo vikuza, lakini kwa Mkwasa, imethibitishwa na zao lake ambalo amelinoa vyema akiwa Ruvu Shooting kabla haijashuka daraja.
Hii ni baada ya kukiri hadi sasa amekuwa akiwasiliana na kocha huyo.
“Nimekuwa chini ya Mkwasa ambaye mbali na kunifundisha kwangu ni mlezi na amekuwa karibu na mimi hadi sasa na amekuwa akinishauri mambo mengi sana pamoja na kunipa imani mimi bado ni mchezaji mzuri na natakiwa kupambana,” anasema na kuongeza;
“Mkwasa kafundisha timu kubwa kama Yanga, anafahamu presha zilizopo kwenye timu zenye mashabiki wengi, amekuwa akinishauri kuwekeza nguvu kwenye upambanaji wangu na hataki kuona nakata tamaa anaamini nina uwezo ni suala la muda tu kupata nafasi ya kucheza.”