Chino Kidd ametoa ujumbe mzito kwa vijana na watu wote, akisisitiza umuhimu wa kumweka Mungu karibu, hasa wakati ambao mtu ana mafanikio. Anasema kuwa kipindi ambacho mtu anasikilizwa na kila mmoja kutokana na ustaa au pesa nyingi, ndicho kipindi bora zaidi cha kufanya matendo mema yanayompendeza Mungu.
Anawaonya vijana wasisubiri hadi wapitie magumu, changamoto, au wapoteze njia ndipo waanze kutoa sadaka au kumkaribia Mungu. Kwa maneno yake, Chino anasema huu si wakati sahihi, kwani wakati huo tayari utakuwa umeshachelewa. Kwa hiyo, anashauri watu wafanye hivyo wakiwa kwenye kilele cha mafanikio yao.
@chino_kidd7 anatoa mfano wake binafsi kwa kusema kwamba, hajawahi kumwambia mama yake amwombee kwa Mungu ili afanikiwe kimaisha. Badala yake, kila anapopata nafasi ya kuzungumza na mama yake, huomba amwombee awe na mwisho mwema. Hii ni kwa sababu yeye anamwamini na kumpenda Mungu, japokuwa anakubali kuwa yeye ni binadamu ambaye hajakamilika.
Pia, anasisitiza kwamba maisha ya duniani ni mafupi sana ukilinganisha na maisha ya mbinguni. Anasema watu wanakufa kila siku, na wengi kati ya hao walikuwa na kila kitu duniani, lakini sasa hatuwaoni tena. Ndiyo maana anatamani kuwa na mwisho mwema, kwa kuwa anaamini maisha ya mbinguni ni bora zaidi kuliko ya hapa duniani.
Kwa ujumla, Chino Kidd ametoa ujumbe wa kutafakari, akiwahimiza vijana na watu wote kumweka Mungu karibu na kufanya matendo mema hata wakati wa mafanikio.