Sean Combs, maarufu kama Diddy, ni msanii na mfanyabiashara maarufu duniani, anayejulikana kwa mafanikio makubwa kwenye muziki na biashara. Hata hivyo, hivi karibuni amekabiliwa na mashtaka mazito yanayoweza kumpeleka gerezani kwa miaka mingi.
Kosa la kwanza ni njama ya uhalifu (racketeering conspiracy), ambapo Diddy anatuhumiwa kutumia biashara zake kama Bad Boy Entertainment na Ciroc kwenye mipango ya uhalifu. Kwa mujibu wa sheria ya RICO, makosa haya yanahusisha vitendo mbalimbali vya uhalifu kama kuhonga kwa dhumuni la kuficha mambo, utekaji nyara, na biashara ya dawa za kulevya.
Pia, Diddy anakabiliwa na kosa la biashara ya usafirishaji wa watu kwa ajili ya ngono. Inadaiwa kuwa aliratibu "Freak Offs," sherehe za siri ambazo wanawake walilazimishwa kushiriki kwenye vitendo vya ngono kwa malipo.
Kosa la tatu ni usafirishaji wa wanawake kwa kusudi la ukahaba, ambapo Diddy alitumia wafanyakazi wake kusafirisha wanawake kwa ajili ya kushiriki kwenye biashara za ukahaba katika sherehe hizo.
Diddy anatuhumiwa kutumia video za ngono za waathirika wa sherehe hizo, kuwamiliki na kuendesha maisha yao, akitishia kuzivujisha ili kuwachafua majina yao, hivyo walilazimika kumtii na kuendelea kumtumikia.
Wasanii na watu wenye vipaji walitishiwa kuharibiwa kazi zao za sanaa kama wangeleta shida, hivyo walilazimika kumnyenyekea ili kulinda nafasi zao kwenye jamii.
Mashtaka haya, ikiwa yatathibitishwa, yanaweza kumpelekea Diddy kifungo cha maisha jela kutokana na uzito wa makosa anayokabiliwa nayo. Hali hii imezua gumzo, huku wengi wakisubiri kujua hatima ya kesi yake.