Wakati Yanga ipo tayari katika ardhi ya Ethiopia kwa mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kocha wa wenyeji ameibuka na mambo matatu mazito aliyoyasoma kwa kikosi hicho cha Jangwani.
Kocha Sisay Kebede Kumbe wa CBE SA ya Ethiopia itakayokutana na Yanga kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Abebe Bikila, jijini Addis Ababa, ameliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu wanakwenda kukutana na timu bora inayoundwa na viungo bora.
Kumbe alisema ubora wa Yanga katikati ya uwanja ni mkubwa na viungo bora akiwamo Pacome Zouzoua, Clatous Chama, Maxi Nzengeli na Stephane Aziz Ki wanaocheza soka la kisasa wakiwa na kasi ya kupokonya mpira kwa wapinzani, pia kushambulia kwa haraka.
Kocha huyo raia wa Ethiopia alisema hatua ya pili ya ubora aliousoma Yanga ni hata safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inayoongozwa na Prince Dube inatengeneza mabao ya kutosha baada ya kuing’oa Vital’O ya Burundi kwa jumla ya mabao 10-0 katika mechi za raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya Afrika.
“Yanga ni timu nzuri, tunakwenda kukutana na mpinzani mwenye mambo mengi mazuri, nimeiangalia timu yao kwanza naweza kusema wanacheza kisasa sana katikati ya uwanja, wana viungo wanaoweka presha kubwa kwa timu pinzani ipoteze mpira lakini hata wakiupata wanashambulia kwa kasi, lazima tujipange sawasawa kuwafanya hawachezi kwa ubora huu,” alisema Kumbe na kuongeza.
“Kitu cha pili ni safu yao ya ushambuliaji, wameitoa ile timu ya Burundi (Vital’O) kwa kuifunga jumla ya mabao 10, hiki sio kitu kidogo. Hii ina maana kama tukifanya makosa kwa ubora wa eneo lao la kati na makali ya washambuliaji wao wanaweza kufanya kitu kibaya kwetu, tumekuwa tukijiandaa na kuhakikisha tunakuwa tayari kupambana na timu ya ubora wa namna hiyo.”
Kumbe aliongeza, rekodi ya Yanga kwenye mashindano ya Afrika ni kitu kingine kinachoufanya mchezo huo kuwa mgumu kwani inatoka kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa huku pia ikifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023.
“Ukiangalia pia rekodi yao kwenye mashindano ya Afrika inathibitisha ni timu bora, msimu uliopita iliishia robo fainali, naweza kusema ilitolewa kwa bahati mbaya lakini ukiangalia nyuma tena unaona walicheza fainali ya Shirikisho.
“Rekodi hizi zinatufanya kuongeza umakini kwenye maandalizi yetu, hatuwezi kuwaogopa lakini nadhani tunatakiwa kujiandaa kucheza kwa ubora dhidi ya timu bora,” alisema.
Alichokisema kocha juu ya ugumu anaotarajia kukutana nao, unajidhihirisha kupitia takwimu za wachezaji wa Yanga katika mechi za kimashindano walizocheza msimu huu.
Yanga ambayo msimu huu imecheza mechi tano za kimashindano zikiwamo mbili za Ngao ya Jamii kama ilivyo Ligi ya Mabingwa Afrika na moja Ligi Kuu Bara, imefunga jumla ya mabao 17 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja pekee.
Katika mabao hayo 17, Prince Dube amefunga matatu, mawili dhidi ya Vital’O na moja dhidi ya Azam katika fainali ya Ngao ya Jamii. Pia ana asisti moja aliyoitoa katika nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.
Clatous Chama amefunga mabao mawili yote dhidi ya Vital’O na kutoa asisti tano, moja Ngao ya Jamii dhidi ya Azam huku nne akipiga katika mchezo mmoja dhidi ya Vital’O waliposhinda 6-0.
Clement Mzize ndiye mwenye mabao mengi akifunga manne, moja Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, mawili dhidi ya Vital’O na moja Ligi Kuu Bara mbele ya Kagera Sugar.
Maxi Nzengeli naye amefunga mabao mawili dhidi ya Simba katika nusu fainalia ya Ngao ya Jamii na lingine Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar.
Aziz Ki amefunga mabao matatu yakiwamo mawili dhidi ya Vital’O na moja fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, pia ana asisti moja aliyoitoa katika Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar.
Mudathir Yahya amefunga bao moja dhidi ya Vital’O na asisti moja akipiga katika fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, huku Pacome akiwa na bao moja alilofunga dhidi ya Vital’O.
Katika mechi zote hizo tano, Djigui Diarra alidaka na kuondoka uwanjani akiwa na cleansheet nne wakati bao moja Azam walijifunga kutokana na krosi ya Chadrack Boka.
SOMA NA HII SIMBA