Licha ya kuanza vyema kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuvuna pointi tatu muhimu dhidi ya wenyeji Kagera Sugar, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamodi, amesema timu yake haikucheza vizuri.
Yanga iliichapa Kagera Sugar mabao 2-0, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba ulioko Bukoba mkoani, Kagera juzi.
Akizungumza na gazeti hili, Gamondi, alisema ameshangazwa wachezaji wake kupoteza nafasi nyingi za kufunga katika mchezo huo ambao ulikuwa kiporo kwa sababu ya mabingwa hao kuwa kwenye majukumu mengine ya kimataifa.
Gamondi alisema kama wachezaji wake wangeongeza utulivu, wangeibuka na ushindi mnono na kujiwekea 'mtaji' kuelekea kwenye mbio za ubingwa ambazo wameanza.
"Nadhani kama tungekuwa makini tungepeta ushindi mkubwa zaidi, hatukuwa vizuri mwenye umaliziaji, tumepoteza nafasi nyingi sana," alisema Gamondi.
Kocha huyo alisema walipoteza zaidi umakini katika dakika 25 za mwisho za mechi hiyo ya raundi ya kwanza.
"Hatupaswi kufanya hivi tena, tutalifanyia kazi kwenye uwanja wa mazoezi, ni muhimu kutumia vizuri nafasi nyingi tunazozipata, muda mwingine mchezo unabadilika kwa sababu wapinzani nao pia huwa wanatafuta matokeo mazuri, lazima tuwe makini, " Gamondi alisema.
Aliongeza kikubwa wanachokifurahia ni matokeo chanya waliyopata kwenye mchezo huo wa ugenini.
"Lengo letu lilikuwa ushindi, tunafurahi tumepata ushindi kwa sababu pamoja na yote, tulijua mchezo huu hautakuwa mwepesi, tulijua Kagera Sugar hawatakuwa wepesi kwenye uwanja wao wa nyumbani, tunashukuru lengo la ushindi limetimia,"alisema Gamondi.
Ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa Yanga ambayo ilikuwa inashiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini ulikuwa ni mchezo wa pili kwa Kagera Sugar.
Ushindi huo umeifanya Yanga kutopoteza mechi ya raundi ya kwanza kwa misimu 10 mfululizo tangu msimu wa mwaka 2014/2015.
Mara ya mwisho Yanga kupoteza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara ilikuwa ni Septemba 20, 2014 ilipofungwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani, Morogoro dhidi wenyeji Mtibwa Sugar, mabao yaliyofungwa na Mussa Hassan 'Mgosi' na Ame Ally.
Simba ndio vinara wa ligi hiyo yenye timu 16, akiwa na pointi sita baada ya kushinda mechi zote mbili walizocheza sawa na Singida Fountain Gate huku Mashujaa FC ya Kigoma ikiwa kwenye nafasi ya tatu na pointi zake nne kibindoni wakati Yanga inafuatia ikiwa na pointi tatu.
Fountain Gate ya Singida iliyopanda daraja msimu huu inafuatia katika msimamo huo ikiwa na pointi tatu sawa na Tabora United ya mkoani Tabora.
Kwa sasa Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kupisha kalenda ya kimataifa ambapo hapa nchini Taifa Stars itawakaribisha Ethiopia katika mechi ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika itakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.