Hatma ya dhamana ya Mwanachama wa Chadema, Mgombea nafasi ya Kanda wa Chama hicho na Meya wa zamani wa Ubungo jijini Dar es Salaam, Boniface Jacob, maarufu mitandaoni kama Boni Yai inatarajia kujulikana leo Jumatatu, Septemba 23, 2024, wakati Mahakama itakapotoa uamuzi wa maombi ya Serikali ya kuzuia dhamana yake.
Mwanasiasa huyo mkazi wa Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam, anakabiliwa na kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo kwenye mitandao ya kijamii.
Alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu Alhamisi Septemba 19, 2024 na akasomewa mashitaka mawili, ambayo hata hivyo aliyakana.
Katika kesi hiyo Boni Yai anakabiliwa na mashitaka mawili yakiwamo kuchapisha taarifa za uwongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.
Alisomewa mashitaka hayo na mwendesha mashitaka Wakili wa Serikali, Nurati Manja.
Katika shitaka la kwanza Wakili Manja alidai kuwa , Septemba 12 2024 jijini Dar alichapisha taarifa za uwongo zikimhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar Es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP).
Taarifa hizo zinasomeka kuwa, "Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kama mtu ambaye ameshiriki mauaji kwa kuwapoteza ndugu wa baadhi ya familia zao, kupotea kwa mfanyabiashara Mussa Mziba, kupotea kwa Deo Mugasa, kupotea kwa Adinani Hussein Mbezi, kupotea kwa vijana watano wa Aggrey."
Katika shitaka la pili Wakili Manja alidai kuwa Boni Yai alitenda kosa hilo Septemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam akidaiwa kuchapisha taarifa za uwongo zinazowahusisha Wakuu wa Upelelezi wa mikoa na utekaji na mauaji ya watu na kutupa miili yao.
Ujumbe huo unasomeka "Mkawasifia Ma-RCO (Wakuu wa Upelelezi Mikoa) wanaozuia uhalifu kwa kutenda uhalifu ...bali Ma-RCO waliokuwa wakiteka, kukamata, kupiga watuhumiwa risasi, kuwafunga tape, kuwafunga mifuko ya nailoni usoni na kisha kutupa miili ya watuhumiwa ndio wanaijua kazi ya upolisi."
Hii ni mara ya pili Boni Yai kupandishwa kizimbani mwaka huu kwa kesi na mashitaka ya aina hiyo