HII HAPA TOFAUTI YA DUBE NA BALEKE
Wataalam wa soka nchini, wamechambua uchezaji wa mastraika wa Yanga, Jean Baleke na Prince Dube, ubora na upungufu walionao, ikitegemea zaidi Kocha Miguel Gamondi anataka nini kutoka kwao, ili kuwatumia kwa mechi tofauti.
Nyota hao wamesajiliwa msimu huu kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya timu hiyo yenye Clement Mzize na Kennedy Musonda na bado hawajapata nafasi ya kuanzishwa pamoja zaidi ya kupokezana uwanjani.
Hata hivyo, mshambuliaji wa zamani wa kimataifa aliyewahi kuzichezea timu tofauti, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ alisema wachezaji hao kila mmoja ana ubora na udhaifu wake na ishu ya kufunga mabao muda utaongea zaidi.
“Dube ana kasi, maamuzi ya haraka, ana changamoto ya kupoteza nafasi, wakati Baleke hana kasi, lakini hakati tamaa, mpambanaji na anajua kukaa eneo la kufunga. Baleke bado hajaanza kupata nafasi ya kucheza, tofauti na Dube, hivyo bado ni mapema, ila huko mbele itajulikana nani anafanya nini,” alisema Mmachinga, huku staa mwingine wa zamani wa timu hiyo, Edbily Lunyamila alisema Dube ana uwezo wa kukupa vitu vingi uwanjani, kama kucheza kama winga na akaacha wengine kucheza kati, anarudi nyuma kasaka mipira na ana kasi, ingawa anakosa nafasi nyingi za kufunga, kutokana na kushindwa kutulia sehemu moja.
“Baleke ni mchezaji anayekaa mbele ya lango ndiyo maana hawezi kukosa sana nafasi za kufunga, mzuri wa kutumia vichwa, japo ana kasi ndogo, kuhusu kutumika kikosini, inategemeana na Kocha Gamondi na mpango wa mechi husika,” alisema Lunyamila.
Tangu Dube ajiunge na Yanga amefunga mabao manne Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Vital’o matatu na moja dhidi ya CBE SA, timu hiyo ikishinda bao 1-0, Ngao ya Jamii fainali dhidi ya Azam alifunga bao moja kati ya 4-1, katika Ligi Kuu bado hajafunga, Yanga ikiwa imecheza mechi moja dhidi ya Kagera Sugar, ambapo yalifungwa na Maxi Nzengeli na Clement Mzize.
Kwa upande wa Baleke, bado hajaanza kupata nafasi ya kucheza ndani ya kikosi hicho dhidi ya CBE aliingia dakika ya 90, ana bao moja dhidi ya Augsburg, Yanga ikifungwa mabao 2-1 huko Afrika Kusini.
Rekodi za Baleke
Msimu uliopita akiwa Simba ambako alicheza nusu msimu kisha kutimkia Al-Ittihad ya Libya, alifunga mabao manane kama aliyoyafunga msimu wake wa kwanza, wakati anajiunga na timu hiyo kwa usajili wa dirisha dogo, akitokea TP Mazembe.
Alitoa asisti moja, alicheza mechi tisa,dakika 443,mipira iliyolenga goli 14, iliyotoka nje ya goli mitano.
Rekodi za Dube
Dube akiwa Azam FC alifunga mabao saba, asisti mbili, mechi 12, mipira iliyolenga goli 17, iliyotoka nje tisa, alicheza dakika 734. Alitoa asisti moja, alicheza mechi tisa, dakika 443,mipira iliyolenga goli 14, iliyotoka nje ya goli mitano.