Sakata la beki mpya wa Singida Black Stars, Israel Mwenda na uongozi wa timu hiyo limebakia hatua chache kabla ya kufikia mwishoni baada ya wasimamizi wa mchezaji huyo kukubali kumlipa Sh 60 milioni ili aungane na timu hiyo.
Mwenda aliyesajiliwa hivi karibuni akitokea Simba baada ya kumalizana na waajiri wake wa Msimbazi, alikuwa bado hajaungana na timu hiyo kwa madai ya kutaka kumaliziwa fedha ya usajili.
Singida imekiri ni kweli hawajafanya hivyo kutokana na makubaliano ya kimkataba kwamba watammalizia fedha hiyo hapo baadae baada ya kuitumikia timu hiyo.
Jana Mwanaspoti liliripoti, Singida BS ilitoa saa 24 kwa mchezaji huyo kuripoti kambini au kuvunja mkataba kwa kuilipa klabu Sh 500 milioni.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Singida BS, Hussein Massanza amesema baada ya kuwasilisha barua kwa viongozi wanaomsimamia mchezaji huyo wamepokea majibu kwamba wamekubali kumlipa mchezaji wao kiasi hicho cha fedha.
"Majibu tuliyoyapata baada ya kuandika barua ni wasimamizi wa mchezaji huyo kukubali kutoa Sh. 60 milion ili mchezaji wao aweze kujumuika na timu tunawapongeza kwa juhudi walizozifanya na uamuzi waliouchukua," alisema na kuongeza;
"Uongozi umeamua kufanya hivyo kwa makubaliano kwamba sisi klabu tutaulipa muda ambao tulikubaliana kulipa mwanzo wa kusaini mkataba ni uamuzi wa busara walioufanya kilicho baki sasa sisi tunasisitiza mchezaji aweze kuripoti haraka kambini."
Masanza alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wachezaji kusoma kwa umakini mikataba yao kabla ya kusaini ili kuto kugeuzwa maswala wanayoombwa kiungwana kuwa sehemu ya mkataba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msimamizi wa mchezaji huyo, Herve Tra Bi wamekiri kweli wapo tayari kulipa kiasi hicho cha fedha ambayo wao watalipwa na Singida BS kwa mujibu wa makubaliano ya kimkataba.