KADA WA CCM MOSHI ADAIWA KUMWAGIWA TINDIKALI

 

KADA WA CCM MOSHI ADAIWA KUMWAGIWA TINDIKALI

Idrissa Makishe, mmoja wa makanda wa Chama cha Mapinduzi(CCM) ambaye anadaiwa kumwagiwa tindikali.

Idrissa Makishe, mmoja wa makanda wa Chama cha Mapinduzi(CCM) ambaye anadaiwa kumwagiwa tindikali.

Watu wasiojulikana wanadaiwa kumvamia na kummwagia kimiminika kinachosadikiwa kuwa tindikali, kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Idrissa Makishe.


Kada huyo mkazi wa Njoro wilayani Moshi amepata majeraha usoni na mikononi na amelazwa katika Hospitali ya Mawenzi.


Msemaji wa hospitali hiyo, Venna Karia, amesema Septemba 20, saa 3.00 usiku walimpokea mgonjwa huyo anayeendelea na matibabu.


"Septemba 20 tulimpokea mgonjwa anayeitwa Idrissa Makishe akiwa amejeruhiwa usoni na mikononi. Inaonekana alimwagiwa kimimimika kisichojulikana ni cha aina gani ambacho kilimsababishia majeraha hayo," amesema.


Alipotafutwa kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa kuzungumzia tukio hilo hakupatikana.


Simulizi ya tukio


Kupitia video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Makishe ambaye ni dereva wa bodaboda amedai tukio hilo lilitokea usiku wa Septemba 20, 2024 eneo la Njoro baada ya kukodiwa na abiria.


Makishe anadai jana (Septemba 20) akiwa kijiweni kwake Kizota, Kata ya Bondeni alikodiwa.


"Aliniambia nimpeleke kwa Mubira nikamwambia poa, wakati natoka pale kijiweni tukiwa njiani tukakutana na bwana mmoja amesimama amevaa shati la bluu bahari akiwa na nyundo na bobo (chupa ya maji) lake kubwa, sasa yule bwana niliyembeba akanambia nimwache pale," anasimulia Makishe.


"Yule niliyekuwa nimembeba akawa anamwambia mwenzake njoo, nikawa nimeshtuka baada ya kumwona ana nyundo na bobo. Wakati ameshuka yule bwana akawa anafungua bobo kama anakunywa maji hivi, nikawa kama nataka kuondoka," anaeleza.


Anadai akiwa anataka kuondoka alimwagiwa maji akahisi kama kuna kitu cha moto kimemwingia mwilini.


"Nilipoenda kupambana nao yule jamaa akanipiga kwa nyundo kichwani, nilikimbia huku napiga kelele kuomba msaada, kila ninayemwomba msaada hakuna anayenisaidia, jicho moja la kushoto likawa linaona kwa shida muda ule, hivyo baadaye nilipata msaada nikaletwa hapa," ameeleza.


Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amelaani akiwataka watu kuacha siasa za kutengenezeana ajali.


Amesema anaamini Jeshi la Polisi litakuja na majibu sahihi juu ya tukio hilo.


"Kama kuna watu wameshaanza siasa za namna hiyo hii ni tofauti kabisa na siasa zinazofanywa na CCM, sisi ni Watanzania, uchaguzi utafika na utafanyika uchaguzi wa haki na siyo wa kumwagiana tindikali au kutengenezeana ajali," amesema Boisafi.


"Niwashauri wanachama wa Chama cha Mapinduzi wafanye siasa safi, hatujafikia mahali tunafanya siasa za chuki. Niwaombe wanachama wawe makini kwenye siasa wanazozifanya na wajue ni watu gani wanaongea nao," amesema.


"Wale watu wanaowahisi wanafanya jambo ambalo siyo sawa watoe taarifa polisi ili waweze kufuatilia na mwisho wa siku ukweli upatikane, Tanzania hii ni yetu sote," amesema.


Si tukio la kwanza


Mwaka 2022 iliripotiwa tukio la mdau wa utalii na mkazi wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Tariq Awadhi kumwagiwa kimiminika kilichosadikiwa kuwa tindikali usoni.


Akizungumza na Mwananchi wakati huo, Tariq alisema tukio hilo lilitokea Machi 5, 2022 akiwa njiani kwenda kula ndipo walipita vijana wawili wakiwa na bodaboda na walipofika karibu yake walipunguza mwendo wakamwagia kitu usoni.


Alisema alipomwagia aligusa uso akahisi kuchomwa, macho yakafumba akapiga kelele kutafuta msaada. Tariq alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad