Wakati Taifa Stars ikitarajiwa kucheza mechi mbili mwezi ujao za kufuzu michuano ya Afcon 2025 dhidi ya DR Congo, washambuliaji wazawa wamezidi kuuwasha moto katika Ligi Kuu Bara, huku kocha wa kikosi, Hemed Morocco akifunguka ya moyoni.
Stars ambayo ilishinda mchezo wa mwisho dhidi ya Guinea kwa mabao 2-1 ikiwa ugenini, ilishuhudiwa mabao yakifungwa na viungo Feisal Salum dakika ya 61 na Mudathiri Yahya ile ya 88.
Kwa muda mrefu, kumekuwa na kilio cha kukosa washambuliaji wanaolijua goli kiasi cha makocha wa Stars kuamua kuwatumia zaidi viungo kusaka ushindi, lakini siku za karibuni washambuliaji wameamka wakiongoza chati ya ufungaji Ligi Kuu Bara.
Washambuliaji ambao wameendelea kukiwasha katika vikosi wanavyocheza na wamekuwa wakipata nafasi mara kwa mata ni Clement Mzize (Yanga) mwenye bao moja katika mechi moja na Nassor Saadun (Azam FC) mabao mawili katika mechi nne akifunga kiufundi mfululizo dhidi ya KMC na Coastal Union.
Yupo pia Seleman Mwalimu wa Fountain Gate ambaye ndiye kinara wa mabao katika ligi akifunga matatu katika mechi nne sawa na straika mwenzake wa timu hiyo, Willium Edgar, ilhali Valentino Mashaka anayeichezea Simba ana mabao mawili aliyofunga katika mechi mbili.
MSIKIE MOROCCO Kocha wa Stars, Morocco alisema washambuliaji hao wamekuwa na mwendelezo mzuri katika ligi na timu zao, lakini hiyo sio sababu ya kuitwa katika kikosi hicho.
Alisema wapo wengi wanaofanya vizuri, lakini kama kocha haangalii rekodi zao pekee. “Tunaendelea kuwafuatilia, hivyo rekodi wanazoziendeleza ni kitu kizuri, ila wanahitaji sana mazoezi zaidi na mechi (za kucheza) ili waweze kushindana na mataifa mengine,” alisema Morocco.