KISA BAO 1 KOCHA GAMONDI AIRUDISHA YANGA DAR USIKU USIKU

 

KISA BAO 1 KOCHA GAMONDI AIRUDISHA YANGA DAR USIKU USIKU

Ushindi wa bao 1-0 ambao haukufurahisha mashabiki wa Yanga, umemfanya kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi kuamua kuirudisha timu Dar es Salaam usiku kwa nia ya kuweka mipango mipya kwa mchezo ujao dhidi ya KMC.


Yanga ilipata ushindi huo mwembamba mbele ya vibonde wa Ligi Kuu KenGold kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya na mara baada ya mchezo huo kikosi hicho kilipanda ndege na kurudi jijini Dr es Salaam.


Uamuzi wa Yanga kurudi fasta Dar umetajwa ni mipango ya kocha Gamondi ambaye hakuona sababu ya kulala jijini Mbeya wakati mbele yao kuna kazi kubwa ya kufanya lakini, huku akiwa anahitaji mabao mengi.


Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa jana Jumatano jioni kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Mara baada ya mchezo huo wachezaji walipumzika kidogo tu, kisha usiku wakaanza safari ya kurudia jijini Dar, hali imeonekana sio ya kawaida lakini Gamondi amefafanua ni kwa sababu ya kuwa na ratiba ngumu mbele yake kutokana na mechi zinazofuatana wakihitaji kufanya vizuri.


Kabla ya mchezo wa jana ulikuwa ni tofauti na matarajio ya wengi ikizingatiwa kuwa, Jumamosi iliyopita usiku Yanga ilikuwa Zanzibar ikicheza dhidi ya CBE SA ya Ethiopia katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kushinda 6-0, ikatinga makundi.


“Jumamosi tulikuwa Zanzibar, Jumapili tukasafiri kurudi Dar, kisha Jumatatu tukasafiri kuja Mbeya jambo ambalo timu imekosa muda mwingi wa kupumzika na kujiandaa kwa mechi," alisema Gamondi na kuongeza;.


“Ratiba inaonekana ni ngumu, lakini ninaifurahia kwani nina wachezaji wengi wanaoweza kucheza kwa kubadilishana na kufanya vizuri.”


Inaelezwa kitendo cha Yanga kutakiwa kucheza mechi tatu ndani ya siku tisa kama ratiba inavyoonyesha, ndio sababu ya Gamondi kuamua kutoilaza timu Mbeya akiamini wakipoteza zaidi muda itawarudisha nyuma katika kufanya vizuri.


“Tunatakiwa kuwa na mwendelezo wa kufanya vizuri, hivi sasa ndiyo kwanza tumecheza mechi mbili, tuna safari ndefu ya msimu katika kutetea ubingwa wetu,” alisema Gamondi.


Baada ya juzi Septemba 25 Yanga kucheza na KenGold jijini Mbeya, Septemba 29 watakuwa Dar es Salaam kupambana na KMC kisha watasalia hapahapa kucheza dhidi ya Pamba Jiji Oktoba 3.


Nafuu ya Yanga imekuja kutokana na mechi mbili zijazo kucheza nyumbani, hivyo Gamondi ameamua kuirudisha timu Dar es Salaam fasta ili kupata muda mwingi wa kujiandaa na mechi hizo ambazo anaziangalia kwa umakini mkubwa ili kurekebisha pale palipoonekana kuna tatizo.


Lakini pia, timu hiyo inasikilizia ratiba ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopangwa Oktoba 7 ili kufahamu wapinzani wake huku mechi za hatua hiyo zikianza kucheza Oktoba hadi Desemba mwaka huu.


Baada ya kurudi Dar es Salaam jana usiku, kikosi hicho leo asubuhi kilipata mapumziko kabla ya jioni kurejea kufanya mazoezi ya ‘recovery’ kisha kesho Ijumaa na Jumamosi ratiba ya mazoezi ikiendelea kama kawaida kabla ya Jumapili kushuka dimbani Uwanja wa Azam Complex kucheza dhidi ya KMC.


Yanga katika mechi mbili za ligi ilizocheza msimu huu, imeshinda zote ikifunga jumla ya mabao matatu dhidi ya Kagera Sugar (0-2) na KenGold (0-1), huku rekodi za msimu uliopita zikionyesha mechi mbili za kwanza ilifunga mabao 10 dhidi ya KMC (5-0) na JKT Tanzania (5-0) ambazo zilicheza nyumbani Uwanja wa Azam Complex.


Nahodha Msaidizi wa Yanga, Dickson Job amezungumzia ushindi mdogo walioupata jijini Mbeya akisema: “Kikubwa tumepata pointi tatu, lakini tulitengeneza nafasi nyingi kipindi cha kwanza na cha pili tukashindwa kuzitumia vizuri.


“Tunashukuru tuliitumia vizuri nafasi moja kufungua na nampongeza mwenzangu (Ibrahim Bacca) kwa kufunga bao hilo kwani inaleta morali kwenye timu.


“Uwanja haukuwa rafiki sana ndio maana tumepata matokeo haya, sasa tunarudi nyumbani ambapo tunakwenda kucheza katika uwanja mzuri, tunaamini tutarekebisha makosa na mabao yatapatikana. Wananchi wasiwe na wasiwasi.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad