Yanga imerejea jana mchana ikitokea Ethiopia ilikokwenda kuvunja mwiko wa kupata ushindi wa kwanza ndani ya ardhi ya nchi hiyo kwa kuichapa CBE SA kwa bao 1-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa, lakini matokeo hayo sio kitu Kocha Miguel Gamondi amegeuka mbogo.
Kocha Gamondi amewawakia wachezaji wa timu hiyo hususani, washambuliaji kwa kushindwa kutumia nafasi walizotengeneza kwenye Uwanja wa Abebe Bikila, Addis Ababa, akisema wamezingua na wanapaswa kusahihisha makosa katika pambano la marudiano litakalochezwa Jumapili ijayo visiwani Zanzibar.
Mashabiki wa Yanga hawakufurahia namna timu hiyo ikitengeneza nafasi nyingi, lakini ikatumia nafasi moja pekee kwa bao alilofunga mshambuliaji Prince Dube na Gamondi naye yuko njia hiyo hiyo akiwawashia moto wachezaji wake akitaka utulivu wanapofika eneo la mwisho.
Gamondi mara baada ya mchezo huo akaanza na Dube akimtaka kuongeza umakini, kisha akarudi kwa timu nzima na amewaambia anataka kuona mabadiliko makubwa kuanzia mchezo wao ujao.
Yanga itarudiana na CBE Jumamosi Septemba 21 pale Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar mechi itakayoamua nani atinge makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza Gamondi alisema hakufurahishwa na hatua ya wachezaji kupoteza nafasi na walistahili ushindi mkubwa wa sio chini ya mabao matano.
Alisema hawezi kulichukulia poa jambo hilo kwani linaweza kuwatibulia hesabu zao msimu huu na amewataka wachezaji wake kila mmoja kubadilika kwa haraka.
“Unawezaje kunyamaza kwa mazingira kama yale, unapotengeneza nafasi unatakiwa kuzitumia kwa wingi, nawaheshimu wapinzani wetu lakini ile ni mechi ambayo tulitakiwa kushinda kuanzia mabao matano,” alisema Gamondi na kuongeza;
“Sio kila wakati utapata nafasi kama zile kisha uje utumie moja, zipo mechi ambazo unaweza kupata nafasi moja au mbili ili uamue mechi, nimewaambia nataka kuona kila mmoja anatuliza akili anapofika eneo ambalo tunatakiwa kufunga.”
Katika mchezo huo Dube aliongoza kwa kupoteza nafasi licha ya kufunga bao pekee ambapo mara baada ya kufunga alionekana akiomba radhi kwa benchi la ufundi kutokana na kupoteza nafasi nyingi, lakini ushindi huo umeifanya Yanga kuandika historia ya kupata ushindi wa kwanza ugenini ikiwa Ethiopia.
Yanga ilishacheza mechi nne za michuano ya CAF na timu za nchi hiyo, lakini iliishia kupoteza mbele na kutoka sare mbili na mara ya mwisho ilikuwa katika mechi ya kuwania makundi ya Shirikisho 2018 ilipolala 1-0 mbele ya Welayta Dicha ila ushindi wa nyumbani wa 2-0 ukawavusha salama.