MAANDAMANO LEO: CHADEMA WASHAURIWA KUKAA MEZA MOJA NA JESHI LA POLISI

 

MAANDAMANO LEO: CHADEMA WASHAURIWA KUKAA MEZA MOJA NA JESHI LA POLISI

Wadau wa demokrasia nchini wamezitaka pande mbili zinazokinzana, yaani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Jeshi la Polisi, kuketi meza moja ili kumaliza tofauti kwa mazungumzo.


Chama hicho kimesema kinataka kufanya maandamano hayo, ili kuishinikiza Serikali kuhakikisha wanachama wake waliopotea wanarejeshwa, wakiwa hai au wafu.


Hata hivyo, Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, David Misime limeshatangaza kupiga marufuku maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika Dar es Salaam, likieleza kuwa yanalenga kuvuruga amani.


Wakizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumapili Septemba 22, 2024, baadhi ya wadau hao akiwamo mwanazuoni na mchambuzi wa sayansi ya siasa, Profesa Ambrose Kessy amesema kuandamana kwa amani ni haki ya kisheria ya wananchi, lakini pia kunaweza kusababisha fujo na kuathiri shughuli za watu wengine kama hayatafanyika kwa lengo lililokusudiwa.


“Kuna watu watashindwa kusafiri, maduka yatafungwa lakini pamoja na kuwa ni haki yao ya kisheria kuandamana ni njia ya mwisho baada ya kujaribu utaratibu mwingine,” amesema profesa huyo.


Amependekeza kuwa ni vyema pande zote zikakaa mezani kwa mazungumzo, kwa kutumia viongozi wenye busara, badala ya kupeleka watu barabarani.


Naye Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo Jumapili, ametoa wito kwa pande zote mbili kutengeneza mazingira ya kufanya mazungumzo ya dhati yanayolenga kupata ufumbuzi sahihi wa mvutao huo.


“Tunaomba Chadema kuahirisha maandamano yao pia tunaiomba Serikali na Polisi kuchukua hatua za kupunguza joto na kutuliza hali ili kujenga mazingira ya mazungumzo ya dhati yanayolenga kupata ufumbuzi sahihi wa mambo yote yanayolalamikiwa na pande zote,”alisema.


Askari Polisi wakiwa katika viunga vya Jiji la Dar es Salaam


Amesema Tanzania inayo hazina ya watu wenye busara na hekima wakiwamo viongozi wa dini ambao wakifanya kazi pamoja, wanaweza kuleta suluhu.


“Tunatoa wito kwa pande zote kutuliza vichwa na kutoa nafasi kwa hekima na busara za uongozi ili zitumike kupata ufumbuzi na suluhisho mwafaka,” alisema


Semu amesema kutokana na mvutano unaoendelea, inawezekana pande zote mbili zina hoja za msingi, lakini tatizo hawajapata fursa ya kufanya mawasiliano yanayostahiki kwa maslahi mapana ya Taifa.


Wakati taarifa ya Semu ikiyasema hayo, Septemba 17, 2024, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba alishauri kuwepo kwa mazungumzo kati ya vyama vya siasa na Serikali ili kuondokana na matatizo yanayolikabili Taifa kwa sasa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi.


Warioba alibainisha hayo Dar es Salaam wakati wa mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kwa lengo la kutathmini hali ya demokrasia nchini, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia inayoadhimishwa kila Septemba 15.


Jaji Warioba alisema kuna matatizo mengi yanatokea lakini pande zinazosigana, hazikutani kuzungumza ili kutafuta suluhisho la changamoto zao.


"Tunayo matatizo lakini hatukutani kuzungumza. Kila mtu anatumia madaraka yake badala ya kukaa na kushauriana," alisema Jaji Warioba ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo wa TCD.


Alihoji: "Hivi hakuna njia ya mashauriano? Kwa mapambano hamuwezi kuleta suluhisho. Bado muda mfupi tunakwenda kwenye uchaguzi, viongozi wote wanaohusika tuwe tumekubaliana. Tukienda kwenye uchaguzi bila makubaliano, zitatokea vurugu, mambo haya ya uchaguzi yanasababisha vurugu. Yaliyotokea mwaka 2001 bado yanapita kichwani, nisingependa yatokee tena," alisema kiongozi huyo mstaafu.


Hali ya Dar es Salaam hadi mchana


Bado Jeshi la Polisi liliendelea kuimarisha ulinzi maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam,huku katika makutano yote ya barabara kuelekea katikati ya mji vikosi vya Polisi viliweka ngome zao.


Katika ngome hizo zilizowekwa maeneo ya Mwenge, Fire,Tazara, Manzese, Daraja la Salenda na Kilwa Road, kulikuwa na magari ya washawasha yakiwa yameangalia upande wa kuingia mjini na wakati mwingine yalikuwa yanafanya doria.


Vilevile katika maeneo hayo kulikuwa na vikosi vya askari Polisi wakiwa wamevalia sare zao na kofia nyendu.


Mwananchi ilishuhudia hali hiyo baada ya kuzunguka maeneo hayo kuangalia hali ya usalama huo ulioanza kuimarishwa na jeshi hilo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad