Mayele Akubali Mziki wa Yanga Adai Itafika Mbali Mashindano ya CAF
Straika za zamani wa Yanga, Fiston Mayele, amekisifu kikosi cha timu hiyo msimu huu, akisema ni kizuri, chenye wachezaji bora wenye njaa ya mafanikio, akikitabiria kufika mbali kwenye michuano ya kimataifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Mayele alisema usajili uliofanyika msimu huu, licha ya kwanza haukuwa mkubwa sana, lakini umeongeza wachezaji bora ambao wameenda kuungana na wengine wenye kiwango cha juu na kuifanya kuwa tishio si Tanzania tu bali Afrika.
Mayele alisema hayo baada ya kumaliza mchezo kati ya Timu yake ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Ethiopia wa kuwania tiketi ya kucheza fainali za Mataifa Afrika (AFCON), mwakani nchini Morocco, uliochezwa juzi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, akifunga bao la pili dakika ya 76, baada ya Theo Bongonda kupachika la kwanza dakika ya 62.
Ethiopia, ambayo walitoka suluhu dhidi ya Tanzania, Jumatano iliyopita kwenye uwanja huo, waliutumia tena safari hii kama wao wa nyumbani kutokana na viwanja nchini mwao kutokidhi viwango vya Shirikisho la Soka Afrika, CAF.
"Yanga imefanya usajili mzuri sana, ina wachezaji wazuri, wanacheza kwa kasi na morali kubwa, msimu uliopita walisajili vizuri na msimu huu pia wamesajiliwa wachezaji wazuri, na hili nimeshawahi kumwambia Rais wa Yanga, Injinia Hersi, nilimpongeza kwa usajili bora na yeye pia alinipongeza kwa kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu nchini Misri.
"Msimu huu wameongeza wachezaji wachache ambao nawatakia kila laheri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu, kama wataendelea kupambana hivi watafanya vema na kufika mbali," alisema Mayele.
Straika huyo aliyeichezea Yanga kuanzia 2021 hadi 2023 kabla ya kuhamia Pyramids ya Misri, amebainisha kuwa inawezekana kuna siku anaweza kurejea Tanzania kwa sababu kwake anaona ni kama nyumbani. "Nimefurahi sana kurudi hapa, Tanzania ni nyumbani, na hata kufahamika zaidi nimefahamika kutokea hapa, Mungu akipenda ipo siku naweza kurejea," alisema.
Mayele pia alibainisha kuwa Ligi ya Misri anakocheza ni ngumu zaidi ukilinganisha ya Tanzania.
"Ligi ya Misri ni ngumu kuliko Tanzania, ina mambo mengi sana hasa kwa wachezaji wa kigeni itakusumbua, pia kule timu karibuni zote unazocheza nazo ni ngumu sana, lakini nimeweza kupambana na nashukuru Mungu kwa sasa nimezoea," alisema straika huyo wa Pyramids, aliyemaliza nafasi ya pili kwenye ufungaji bora nchini humo akiwa na mabao 14, nyuma Wessam Abou Ali wa Al Ahly, raia wa Palestina aliyemaliza na mabao 18.