Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa Freeman Mbowe amesema kesho Septemba 9, 2024 wanatarajia kupata ripoti kamili ya uchunguzi wa mwili wa aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chama hicho, Ali Kibao kutoka Jeshi la Polisi na kuwa endapo ripoti hiyo ikiwa tofauti na wanavyoamini wataipinga.
Mbowe ametoa kauli hiyo jana Septemba 8, 2024 jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Mwananyamala Wilayani Kinondoni, alipofika akiwa na viongozi wengine wa Kitaifa baada ya kupata taarifa kuwa mwili wa mwanachama huyo upo Hospitalini hapo, siku chache baada ya kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana.
Aidha, Mbowe amesema baada ya kupokea taarifa ya Polisi Chadema itaamua ni jambo gani litakwenda kufanya, huku akivituhumu vyombo vya dola katika tukio hilo.
"Tumeshauriana na familia ikakubali wanasheria wa Chama washiriki Pamoja na madaktari katika kuuchunguza mwili wa Ali Kibao ili tujue ameuwawa kwa namna gani. Uchunguzi umeshafanyika na ni dhahiri kwamba Ali Kibao ameuwawa baada ya kupigwa sana na hata kumwagiwa tindikali katika uso wake," ameeleza Mbowe.
Mbowe amerudia rai yake ya kutaka kuundwa kwa Tume ya kijaji kuchunguza matukio ya utekaji yanayoendelea kurindima nchini.
"Wote sisi ni watu ambao maisha yetu yapo hatarini, yeyote kiongozi wa CHADEMA Maisha yake yapo hatarini. Rais anapaswa atoke atoe kauli juu ya hili jambo na aliundie Tume ya Kijaji ya Mahakama kwa sababu Polisi hawana uweledi wa kuchunguza jambo hili hata kidogo," alisisitiza Mbowe.
"Kama chama tulikubali pamoja na wanafamilia katika kufanyia Uchaguzi mwili wa Kiongozi wetu Kibao ,Taarifa zinasema alipigwa sana na kumwagiwa Tindikali Usoni" Freeman Mbowe.
Kibao ni mmoja wa mashujaa wa vita ya Kagera. Baada ya kustaafu Jeshini, Kibao alingia katika kufanya biashara na pia kufanya kazi na vyama mbalimbali ikiwemo CCM, alifariki akiwa mjumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA.