Mchezaji Yusuph Kagoma Agoma Katu Kuwaomba Radhi Yanga Hadharani




MWENYEKITI wa Chama cha Wachezaji wa Mpira wa Miguu Tanzania, (SPUTANZA), Mussa Kisoki, ameibuka na kusema mchezaji Yusuph Kagoma hapaswi kumuomba msamaha mtu au klabu yoyote kwa kilichotokea na kufanya hivyo ni kumdhalilisha.

Kisoki alisema hayo kutokana na Klabu ya Yanga, kupitia kwa Ofisa Habari wake, Ali Kamwe, kumtaka mchezaji huyo kuomba msamaha kwa alichowafanyia ili wamruhusu kuichezea klabu yake ya sasa, Simba.

Yanga imepeleka shauri kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji juu ya mchezaji huyo kuwa alichukua pesa zao na kusaini mkataba, lakini baadaye wakasikia amesaini tena kwenye Klabu ya Simba.

Hata hivyo, Kamwe alidai ili wamwachie wanataka mchezaji huyo aombe radhi, la sivyo watamhesabu kama ni mchezaji ambaye amesaini pande mbili.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kisoki alisema kwa jinsi alivyolishughulikia suala hilo tangu Ijumaa iliyopita na vielelezo alivyoletewa, Kagoma hapaswi kumuomba mtu au klabu yoyote msamaha na yeyote anayetaka hivyo, basi nia yake ni kumdhalilisha mchezaji.

"Tumeanza kulishughulikia suala la Kagoma tangu Ijumaa na tumepata vielelezo vinavyoonesha suala hili halikuhitajika liwe la muda mrefu kiasi hiki, lilitakiwa limalizike tangu huko nyuma, lakini kuna watu wanataka kutunishiana misuli tu kwa ajili ya mchezaji.

"Kagoma alikuwa mchezaji wa Fountain Gate sasa ukienda kwenye kanuni za shirikisho zinazoongoza ligi, kuna kanuni ya 59 ya uhamisho ambayo yeye anaingia hapo, haingii kama mchezaji anayemaliza mkataba wake, au yupo huru anatoka kwenye klabu, anaamrishwa na klabu nini cha kufanya, hakuna kosa lolote alilofanya Kagoma, kila alilokuwa akifanya ni kwa maelekezo ya klabu," alisema Mwenyekiti huyo.

Alisema kuanzia leo ataanza kutoa taarifa rasmi kuhusu tukio hilo, lakini akasisitiza kuwa Kagoma hana kesi yoyote ya kujibu kwa sababu kila kitu kilikwenda kama kilivyopangwa.


"Kwa leo niishie hapa kwa sababu bado naendelea kupata vilelelezo, kesho nitaanza kutoa taarifa rasmi, ila naishia kusema hapaswi kumuomba mtu yeyote msamaha kwa sababu alikuwa mali ya klabu, ndiyo maana hata hao waliomfuata mchezaji walianza kuongea na klabu yake baada ya kupata baraka wakaenda kuongea na mchezaji.

"Sasa kama hakukuwa na maridhiano huwezi kusema mchezaji ambaye hakuwa wa kwako aombe msamaha, kwetu sisi tunaona ni kumdhalilisha mchezaji," alimaliza Mwenyekiti huyo wa SPUTANZA.

Inadaiwa kuwa Kagoma awali aliongea na Yanga, lakini baada ya kuchelewa kumtimizia mahitaji yake kwa muda ambao waliwekeana, alisaini Simba ambao waliilipa klabu yake na mchezaji mwenyewe, huku Fountain Gate pia ikitoa barua ya kumruhusu kujiunga na timu mpya.

Kwa sasa suala hilo lipo kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji huku akizuiwa kucheza mpaka litakapomalizika, licha ya kwamba alikuwa ameshacheza mechi moja ya Ligi Kuu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad