Mmiliki Mwingine wa Mabasi Afariki Duniania Akiendesha Basi Lake...



Picha ikimuonyesha aliyekuwa mmiliki wa mabasi ya A-N Coach, Amduni Nassor mkazi wa Tabora akipanda kwenye moja ya mabasi yake wakati wa uhai wake.

Mwezi mmoja baada ya aliyekuwa mmiliki wa mabasi ya Sauli, Solomon Mwalabhila kufariki dunia, majonzi yametawala tena baada ya aliyekuwa mmiliki wa Kampuni ya AN Coach, Amduni Nassor kufariki dunia katika ajali ya gari iliyoua watu 12 na kujeruhi wengine zaidi ya 36.

Agosti 5, 2024 simanzi ilitawala kutokana na kifo cha Mwalabhila aliyekuwa Mkurugenzi wa kampuni ya Sauli ambaye gari alilokuwa akisafiria liligongwa kwa nyuma na lori la mchanga eneo la Mlandizi mkoani Pwani. Mtoto wake aliyekuwa naye alipata majeraha.

Leo Septemba 6 alfajiri, mwekezaji katika sekta ya usafiri na usafirishaji, Nassor ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya AN Coach amefariki dunia katika ajali ya basi lake iliyotokea eneo la Luanjiro, Mbeya Vijijini.

Ajali ya basi hilo lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Tabora likiendeshwa na Nassor, imetokea ikiwa ni siku mbili zimepita baada ya nyingine kutokea Septemba 4, katika Kata ya Chimala, wilayani Mbarali mkoani hapa ikihusisha basi la Kampuni ya Shari Line iliyosababisha vifo vya watu tisa na kujeruhi wengine 18.

Ajali basi la AN

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema katika ajali ya basi la AN, watu 12 wamepoteza maisha papo hapo, huku zaidi 36 wakijeruhiwa, watano wakiwa katika hali mbaya na wamepelekwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.


Basi la Kampuni ya A-N Coach baada ya kupata ajali katika eneo la Luanjilo Wilaya ya Mbeya Vijijini leo Septemba 6, 2024.
Amesema majeruhi wengine wamesambazwa katika vituo vya afya tofauti vikiwamo vya Chalangwa na Chunya Mjini.

"Chanzo ni dereva wa gari ambaye alikuwa mwendo kasi katika eneo hilo lenye kona kali, gari liliangukia ukutani likafunika bampa la juu na kuwabana wananchi na kusababisha vifo na majeruhi hao," amesema.

"Tunaendelea kufanya utaratibu kwa wananchi walio na uhusiano na watoto sita ambao wamepoteza wazazi wao waweze kuja kuwachukua kwa kuwa wengi ni miezi miwili, mitatu, mitano na saba," amesema Homera.


Amesema baada ya ajali hizo amesema lazima wachukue hatua kwa mamlaka zote kukutana kujadiliana namna ya kudhibiti ajali, huku hatua za haraka ni kuweka mabango makubwa maeneo yote yenye changamoto za ajali na matuta. Amesema mabasi yaliyohusika na ajali hayakuwa na vidhibiti mwendo.

"Mamlaka zote zinazohusika na mambo ya barabarani wakutane haraka kuweka mkakati wa kudhibiti ajali hizi, kwani watu 21 wamepoteza maisha juzi na leo," amesema.

Katika kudhibiti ajali amesema magari yanapaswa kukaguliwa na mabovu hayapaswi kufanya kazi.


Ameelekeza Jeshi la Polisi kufanya ukaguzi wa magari yote yanayosafiri zaidi ya kilomita 200 lazima yawe na madereva wawili na watakaokiuka utaratibu wachukuliwe hatua kali.

"Latra Mkoa wa Mbeya lazima wajitathmini kwa kushindwa kudhibiti magari yasiyo na vidhibiti mwendo, magari yote mabovu yasifanye kazi mkoa wetu na wananchi watoe taarifa kwa dereva anayeendesha mwendo mkali," amesema.

Ameelekeza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mbeya kuweka mabango makubwa kuelekeza hatari ya eneo hilo kuwa na kona kali na kwamba sehemu hiyo ya ajali ilikuwa ijengwe kwa kukatiza mlima lakini palitokea mabishano baina ya mkandarasi na wananchi.

"Taratibu za kihandisi zinafanyiwa kazi ili kuepusha ajali," amesema.

Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wasafirishaji Stendi Kuu Mbeya, Noah Mwashela amesema wamepokea taarifa ya kifom cha Nassor kwa majonzi.

Amesema kupitia uwekezaji wake alitengeneza ajira kwa vijana.

Amesema Nassor alikuwa na utaratibu wa kuwatembelea mara kwa mara hapo stendi akiwa na gari binafsi, lakini ana taaluma ya udereva na mara nyingine alikuwa akiendesha mabasi kumsaidia dereva wake.

"Tumepata taarifa hizo kwa masikitiko hadi wakala wake hapa stendi kuu amezimia na kupewa huduma, alikuwa na utaratibu wa kuja mara kwa mara hapa, kwa kuwa kwao ni Tabora," amesema.

"Alikuwa na gari lake binafsi na hilo basi lililopata ajali lina dereva wake japokuwa muda mwingine alikuwa akiendesha yeye akimpokea mfanyakazi wake ila walikuwa wakisafiri wote," amesema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad