Profesa Karim Manji wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) amechaguliwa kuwa miongoni mwa washindi wa tuzo ya mhitimu bora wa Chuo Kikuu cha Harvard.
Tuzo hiyo inayotambulika kwa jina la 'Harvard T.H Chan School of Public Health Alumni Merit Award 2024' hutolewa kwa aliyewahi kuwa mhitimu wa chuo hicho mashuhuri kwa wanafunzi ‘vipanga’ duniani na aliyejitoa kwa ajili ya afya ya jamii.
Profesa Manji akiwa Mtanzania wa kwanza kuwahi kupata tuzo hiyo, ataipokea Septemba 27, 2024, mjini Boston, Marekani.
Katika taarifa za pongezi zilizotolewa na Muhas katika mitandao ya kijamii leo Jumamosi Septemba 14, 2024, Profesa Manji ni mtafiti mkuu wa magonjwa ya watoto na maisha yake mengi ya taaluma amejikita kusaidia jamii katika eneo hilo.
"Profesa Manji ni mashuhuri na mtafiti mkuu wa magonjwa ya watoto na afya ya mtoto, katika maisha yake yote, amejitahidi kutoa huduma ya kipekee inayomlenga mgonjwa na kufanya utafiti wa kimsingi kuhusu lishe ya watoto, magonjwa ya kuambukiza, na changamoto za ukuaji wa mtoto," imesema taarifa hiyo.
Pia, katika taarifa imeongeza: "Profesa Manji ametoa machapisho 260 yaliyosaidia jamii na watu wa umri mbalimbali, amefanya majaribio kadhaa ya kimatibabu na miradi ya utafiti iliyofadhiliwa.’’
Taarifa hiyo imeongeza kuwa mchango wa Profesa Manji umesababisha mabadiliko ya sera na miongozo ya matibabu kwa watoto nchini.