MWAMBA ASOTA GEREZANI MIAKA 46 AKISUBIRI KUNYONGWA KWA KOSA AMBALO HAKUTENDA

 

MWAMBA ASOTA GEREZANI MIAKA 46 AKISUBIRI KUNYONGWA KWA KOSA AMBALO HAKUTENDA

Unaujua msemo unaosema sheria duniani haki mbinguni? Iwao Hakamada, mwanaume mwenye umri wa miaka 88 kutoka nchini Japan, ameweka historia ya kuwa mfungwa aliyekaa akisubiri hukumu ya kifo kwa muda mrefu zaidi duniani, akiwa amekaa miaka 46 gerezani na miaka mingine 10 uraiani kabla ya leo, Septemba 26, 2024 kubainika kwamba kumbe alihukumiwa kunyongwa kimakosa.


Hakamada aliyekuwa bondia wa zamani, alikamatwa na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa mwaka 1968 baada ya kukutwa na hatia ya kumuua bosi wake, mke wa bosi huyo, na watoto wao wawili wa kiume.


Baada ya hukumu hiyo, Hakamada alianza kusubiria hukumu yake ya kunyongwa kama wafungwa wengine wanaohukumiwa adhabu hiyo nchini Japan ambapo alitenganishwa na wafungwa wengine wa kawaida, na maisha yakaendelea, kila siku akiwa hana uhakika kama atayaiona mapambazuko ya kesho yake kabla ya kupigwa kitanzi.


Kila mtu alimkatia tamaa Hakamada, isipokuwa dada yake, Hideko ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 91 ambaye aliendelea kumpambania mdogo wake, akiwa na imani kubwa kwamba ipo siku ukweli utafahamika kwamba ndugu yake hakuwa amehusika na mauaji hayo.


Mwaka 2014, hatimaye rufaa ya Hakamada iliyokatwa na dada yake, ilipewa nafasi ya kusikilizwa baada ya kuwa imepigwa danadana kwa miaka mingi. Mungu si Athuman, baada ya kukubaliwa kwa rufaa hiyo, Hakamada aliachiwa kutoka gerezani lakini bado kesi haikuwa imefutwa isipokuwa ushahidi ndiyo haukutosha kumfanya aendelee kukaa gerezani.


Miaka kumi baadaye, hatimaye Mahakama ya Wilaya ya Shizuoka chini ya Jaji Koshi Kunii imeamua kufuta mashtaka hayo na kueleza kuwa ushahidi uliotumika kumtia hatiani Hakamada, ulikuwa wa kutengenezwa na kwamba aliteswa na polisi na kulazimishwa kukubali kitu ambacho hakukifanya.


Kutokana na matatizo ya kiafya aliyoyapata tangu akiwa gerezani, Hakamada hakuwepo mahakamani wakati mashtaka dhidi yake yakifutwa na badala yake, amewakilishwa na dada yake, Hideko ambaye ndiye aliyekuwa akimpambania kwa kipindi chote hicho!


Umejifunza nini kutokana na tukio hili?

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad