Wakili, Peter Madeleka. Picha na Mtandao
Dar es Salaam. Hatua ya baadhi ya wananchi kujitokeza na kumchangia mamilioni ya Shilingi Wakili maarufu, Peter Madeleka kwa ajili ya kuendelea na kesi ya anayetajwa ‘afande’ jijini Dodoma, imeelezwa kuwa inaonyesha kiu ya haki ilivyo kubwa miongoni mwa wananchi.
Shauri hilo la malalamiko namba 23627 dhidi ya Fatma Kigondo anayetajwa kama ‘Afande’, lilifunguliwa na Wakili Paulo Kisabo na kupangwa mbele ya Hakimu Mkazi Francis Kishenyi Septemba 5, 2024.
Hata hivyo, Wakili anayemwakilisha Kisabo, Madeleka hakuweza kufika mahakamani siku hiyo kutokana na alichokiandika katika ukurasa wake wa X kwamba amekosa fedha.
Kesi ya Afande imeitwa leo tarehe 5 Septemba 2024 kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, lakini nasikitika nimeshindwa kwenda kutokana na ukosefu wa fedha za kuendesha kesi hiyo,” kauliambayo imewaibua mashabiki zake na kuanza kumchangia.
Akizungumza na Mwananchi leo asubuhi Septemba 7, 2024, Madeleka amesema hadi jana mchana alikuwa amepokea Sh19 milioni na bado michango inaendelea kumiminika.
Ilipofika saa 8 mchana ameandika kwenye ukusara wa X kuwa ameshachangiwa zaidi ya Sh73.15 milioni.
“Hizo ni fedha ambazo zinachangwa na watu wasiofurahishwa na uhalifu na ndio inavyotakiwa katika utafutaji haki. Unajua watu wanataka matokeo, lakini wengine hawako tayari kuchangia,” amesema.
Hata hivyo, amesema fedha hizo hazichangwi kwa ajili ya kugharamia kesi, bali kwake binafsi wakiunga mkono juhudi zake.
Akizungumzia michango hiyo, Wakili John Seka amesema inaonyesha kuwa watu wana kiu ya haki, “Kwa hiyo kama mtu amejitokeza kuwatetea, lazima watampa msaada.”
Amesema katika fani ya sheria, watetezi wa haki za binadamu ni wachache na eneo hilo linakimbiwa na wanasheria kwa kuwa linaonekana halina masilahi.
“Watetezi wa haki za binadamu sio wengi na sio filed (eneo) ya watu kupata faida, hivyo wengi wanaikwepa, kwa hiyo inapotokea wanaojitokeza kutetea wananchi, watu watawaunga mkono,” amesema.
Kauli hiyo imeungwa mkono na mwanasaikolojia Jacob Kilimba alipoulizwa kuhusu suala hilo, akisema michango hiyo inaonyesha kiu waliyonayo wananchi kwa ajili ya haki.
“Kwa sasa kuna watu wengi wanafanyiwa vitendo vya ukatili na hawana mahali pa kupatia haki, sasa anapojitokeza mtu aliyejitolea kuwatetea, lazima wamuunge mkono.
“Kuna wengine wana mambo magumu moyoni, hivyo anapotokea mtu wa kuwatetea, wanayatoa ya moyoni kupitia mtu huyo,” amesema.
Mbali na kesi ya ‘Afande’, Madeleka amehusika pia kwenye kesi ya marehemu Stella Moses aliyedaiwa kujinyonga akiwa mahabusu ya kituo cha Polisi Mburahati Dar es Salaam Desemba 20, 2020.
Pia, Madeleka alimwakilisha Hashim Ally katika kesi dhidi ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria na mbunge Babati Mjini, Pauline Gekul, ambapo alidai kufanyiwa shambulio la kudhuru mwili na kiongozi huyo Novemba 11, 2023.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliifuata kesi hiyo akieleza kutokuwa na nia ya kuendelea nayo.
Nyingine ni kesi ya vijana wa Bavicha waliotekwa Temeke, Dar es Salaam, Deusdedith Soka na wenzake wawili shauri ambalo Agosti 28, 2024 Mahakama Kuu Masjala ya Dar es Salaam ilitoa uamuzi kuwa, hakuna ushahidi kuwa, vijana hao wanashikiliwa na Polisi lakini jeshi hilo likapewa amri ya kuwatafuta.
Akizungumzia hilo, mwanaharakati Tito Magoti amesema, “anachofanya Madeleka ni uhamasishaji wa wananchi kwa ajili ya kesi zenye masilahi ya umma.”
Amesema si ajabu kuona wanasheria wakiomba michango kwa kuwa hata taasisi nazo hupata michango ya wafadhili.
“Kwa taasisi zilizosajiliwa zinapata ufadhili moja kwa moja na pia zinachangisha fedha. Kwa mtu mmoja mmoja pia wanachangisha.
“Uhamasisha wa haki za binadamu ni jukumu la kila mmoja,” amesema.
Utaratibu wa TLS
Akizungumzia uchangishaji huo, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi amesema japo chama hicho kina utaratibu wa msaada wa kisheria, lakini una mlolongo mrefu, hivyo alichokifanya Madeleka ni njia sahihi.
“Kwanza ujue hiyo (ya TLS) ni michango ya mawakili wenyewe, sio kwamba Serikali ndio inatoa au labda kuna mfadhili mwingine. Pia ni lazima anayetaka msaada alete maombi kwa maandishi na kuna kamati inayomjadili kuona kama anastahili kusaidiwa au la.
“Kwa hiyo utaratibu upo, lakini tunaangalia na uwezo wa bajeti yetu,” amesema.
Mwabukusi amesema njia anayotumia Madeleka ni nzuri zaidi ili kuharakisha utetezi kwa wananchi.
“Watu wengi wanashindwa kesi kwa sababu wanakosa utetezi na hawana fedha, hivyo wakili akijitokeza kuwatetea na hana nauli, kuna shida gani kumchangia?
“Kama watu wanachangia harusi ambayo hawapati kitu, kwa nini wasichangie watu kupata haki?” amehoji.