NAMNA LIPA NAMBA INAVYORAHISISHA MALIPO KIDIGITALI

 

NAMNA LIPA NAMBA INAVYORAHISISHA MALIPO KIDIGITALI

Miongo miwili iliyopita isingeweza kufikirika kuwa itafika wakati katika maisha mtu ataweza kulipia bidhaa au huduma anayonunua kwa urahisi kiasi cha kupangusa tu katika simu yake ya kiganjani.


Kwa sasa hili ni uhalisia, kuwepo kwa mtindo wa malipo kupitia Lipa Namba kumeleta urahisi mkubwa wa kulipia bidhaa na huduma katika sehemu mbalimbali za biashara nchini.


Lipa Namba ni mfumo wa malipo kidijitali au kielektroniki uliobuniwa na makampuni ya huduma za mawasiliano simu za mkononi, ambapo kwa wafanyabiashara kwenye maeneo yao mbalimbali ya biashara zao wanaweza kupokea malipo kwa urahisi kutoka kwa wateja wao kupitia mfumo wa namba maaalumu ya malipo kwa njia ya simu (Merchant Code/Lipa Namba).


Kufikia mwaka jana 2023, jumla ya wafanyabiashara 607,599 walikuwa wamejiandikisha kutumia mfumo huo, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 76 ikilinganishwa na idadi ya wafanyabiashara 345,219 mwaka mmoja uliopita.


Sambamba na hilo, idadi ya miamala iliyofanyika kwa Lipa Namba na malipo kibiashara imeongezeka pia, mwaka 2023 miamala milioni 280.79 yenye thamani ya Sh15.8 trilioni imefanyika kwa mfumo huo, sawa na ongezeko la asilimia 83 ikilinganishwa na idadi ya miamala iliyofanyika mwaka uliopita 2022.


Kwa mujibu wa taarifa ya BoT kuhusu Mwenendo wa Mifumo ya Malipo nchini (Tanzania Payment Systems, Annual Report, 2023), mwenendo huo wote kwa ujumla unaonesha kuwa mtindo huo wa malipo unakua kwa haraka, idadi ya watumiaji na miamala inayofanyika inaongezeka kwa zaidi ya asilimia 70 kwa kipindi cha mwaka mmoja tu.


Zipo sababu kadhaa zinazoweza kuwa zimechangia kukua kwa mtindo huo ambapo ya kwanza iko upande wa mteja, kwani ni rahisi kutumia, anaweza kulipia bidhaa au huduma aliyopata bila kuhitaji kubeba fedha taslimu, inampa urahisi wa malipo ya haraka.


Kitu cha pili ni kutokuwa na wasiwasi kuhusu usalama wake, au kupoteza fedha alizobeba.


Kwa upande wa mfanyabiashara inamuepusha kukaa na fedha nyingi taslimu dukani, kwa mfano maduka ya jumla, wanaweza kuwa na fedha taslimu kiasi kikubwa kwenye droo za kuhifadhia, kupokea malipo au kutoa chenji, jambo ambalo kwa usalama wao si zuri, hivyo Lipa Namba inaweza kusaidia kuondoa adha hiyo.


Hata hivyo, changamoto bado zipo, kwani uelekeo huu wa maendeleo ya mfumo wa malipo kidijiti unafaidisha zaidi wakazi wa maeneo ya mijini, mfano, karibia nusu ya watumiaji wa Lipa Namba wapo katika mikoa minne ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha.


Hii inatoa picha kuwa ingawa mwenendo wa ukuaji wa huduma hiyo ni mzuri, bado sehemu kubwa ya wafanyabiashara na wateja wako nje ya mfumo huo au tuseme hawautumii.


Sambamba na hilo, si wafanyabiashara au wananchi wote wenye uelewa wa namna ya kutumia huduma hiyo, mfano, labda kutokana na uelewa mdogo wa matumizi ya vifaa vya kiteknolojia au mifumo ya teknolojia ya malipo, hivyo wengine inawezekana hawajaamua kutumia kutokana na wasiwasi kuhusu usalama wa fedha zao mtandaoni, hofu kuhusu makato ya tozo, au mengine.


Kufuatia hili, ni vyema Serikali, makampuni ya utoaji wa huduma za simu na wadau wengine wanaotoa huduma za kifedha waendelee kuwekeza katika kutanua upatikanaji wa huduma za mtandao wa simu na intaneti zaidi katika maeneo ya miji midogo na vijijini kuwezesha watu wengi zaidi kufikiwa na kutumia huduma hii.


Aidha, programu za mafunzo kwa wananchi, wafanyabiashara ziendelea kufanyika kuelimisha umuhimu wa huduma kama hiyo, namna ya kuitumia, na huduma nyingine za malipo kwa mfumo wa kidijitali ili watu wengi zaidi waweze kutumia na kuongeza idadi ya ujumuishi wa huduma za kifedha nchini.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad